Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Jengo la Yanga, Francis Kifukwe amesema kituo cha mabasi yaendayo kasi (DARTS) kilichojengwa eneo Jangwani kipo ndani ya eneo lao, haya maneno kayatoa wakati wa ziara ya Kamati ya Mipango Miji na Mazingira ya Manispaa ya Ilala ikiwa ni ziara ya ukaguzi Jangwani kuangalia eneo linaloombwa na klabu ya Yanga kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wake wa kisasa.
Kifukwe alionyesha eneo wanalohitaji kuongezewa mbele ya Kamati ya Mazingira kuwa eneo lao linafika hadi kwenye kituo cha mabasi ya mwendo kasi akidai kuwa waongezewe mpaka kwenye bonde la Mto Msimbazi.
“Kile kituo cha mabasi tumeambiwa kipo pale kwa muda, kwa upande huu tutafika mpaka sehemu ya matairi (karibu na bonde Msimbazi) na upande huu wa Barabara ya Morogoro mwisho wa mpaka wetu ni kwenye misufi lakini tunaomba mtuongezee mpaka kule barabarani kabisa.
Kwenye sentensi nyingine alisema “Mtuzidishie barabarani kwa vile upande huu wa mbele tayari kuna barabara ya kiwango cha lami imejengwa ambayo inaenda mpaka Kigogo na inatumika na watu wengi hivyo hii barabara hatutaigusa, na upande huu wa Barabara ya Morogoro kuna bomba jingine ambalo litaingia ndani ya uwanja wetu.”
Baada ya hayo, mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji na Mazingira ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Upanga Mashariki Sultan Salum, alisema wamepokea maombi ya Yanga na wameona eneo wanalohitaji hivyo watakaa kikao Jumanne ijayo kujadili na kujiridhisha iwapo itafaa.
Amekaririwa akisema “hili suala lina mlolongo mrefu kwa sababu sio NEMC tu itabidi liende mpaka kwa watu wa ardhi na Serikali Kuu, sio la kumalizika leo hili.. sisi Jumanne tutakaa wajumbe watakavyoamua tutawapa majibu.”
Hata hivyo tayari ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Manispaa ya Ilala wameshaweka wazi msimamo wao wa kuwataka viongozi wa Yanga kubeba dhamana ya fidia za watakaoathirika na ujenzi wa uwanja huo na kwamba gharama halisi itajulikana itakapofanyika tathmini halisi.
SOURCE: MWANANCHI