Wananchi wa Zambia wanasherehekea maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru siku ya leo, huku rais wa nchi hiyo Michael Chilufya Sata akiwa nje ya nchi anakotibiwa.
Hii ni mara ya kwanza kwa rais huyo anayefahamika kama King Cobra kutoshiriki katika maadhimisho ya kumbukumbu hiyo tangu aingie madarakani mwaka 2011.
Taarifa za kuugua kwa Sata zimekuwa zikienea kwa kipindi kirefu ambapo kuna wakati alilazimika kuhutubia bunge la nchi hiyo na akisisitiza kwamba hajafariki kama ambavyo ilikuwa ikidhaniwa na watu wengi baada ya kutoonekana hadharani kwa kipindi kirefu.
Wasi wasi juu ya afya ya rais Sata ulitanda pale aliposhindwa kuhutubia katika kikao cha umoja wa mataifa UN, na baada ya kurejea nchini humo alitangaza rasmi kuwa anasafiri kwa ajili ya kwenda kutibiwa nje ya nchi japo hakuweka wazi anakwenda kutibiwa nchi gani.
Hii ni mara ya kwanza kwa rais huyo kukosekana katika maadhimisho ya siku ya uhuru tangu aingie madarakani mwezi Septemba 2011.
Mataifa mbali mbali pamoja na Marekani, Uingereza na Ufaransa wameipongeza Zambia kwa kudumisha amani na demokrasia huku wakiahidi kuendeleza ushirikiano uliodumu baina ya mataifa hayo kwa kipindi chote cha miaka 50 tangu nchi hiyo ipate uhuru.