Ofisa mtendaji mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula (NFRA) Milton Lupa amesema Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua mradi wa vihenge na Maghala ambao umejengwa wilayani Babati mkoani Manyara Novemba 22.
Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Babati kwenye eneo la mradi amesema katika mradi huo vimejengwa vihenge nane vya kisasa ambavyo vina uwezo wa kuhifadhi tani 25,000 ambapo umetumia gharama sh. Bil. 19.359 mpaka kukamilika kwake na utasaidia kuhifadhi tani 40,000 za mazao ambapo ulijengwa na mkandarasi UNIA kutoka nchini Poland kwa kusaidiana na mkandarasi mzawa kutoka jijini Arusha.
Lupa ametaja kazi zilizofanyika kuwa ni ujenzi wa vihenge vya kisasa nane, ujenzi wa majengo ya utawala, stoo na maabara, ujenzi wa barabara za ndani na kusimika mifumo ya kielekroniki.
“Hivi vihenge vinatumia teknolojia ya kisasa ambapo mahindi yataweza kuhifadhiwa kwa zaidi ya miaka mitano”- amesema Lupa
Ofisa mtendaji mkuu huyo amesema licha ya mkandarasi huyo kufanya ujenzi wa mradi ametoa ajira kwa vijana wa kitanzania ambao wengine amewapeleka nchini Poland wafanye kazi ili waje na ujuzi wa kuisaidia Nchi na wengine wamebaki kwenye mradi ili kusaidiana na wataalamu wa NFRA.
Amewaomba wananchi kuhudhuria kwenye uzinduzi wa mradi huo utakaofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kesho Novemba 22.