Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Exhahudi Kigahe amesema bei za vyakula kwa mwezi December mwaka huu zimeendelea kupanda kutokana na vita inayoendelea baina ya Nchi ya Urusi na Ukraine huku akibainisha kuwa sio tu Tanzania tu bali na Mataifa mengine pia huku majanga mengine ikiwa ni ukame ulioathiri mazao ya chakula
Kihage ameyasema hayo Jijini Dar es salaam leo wakati akieleza mwenendo wa bei za bidhaa muhimu nchini kwa mwezi December 2022 na kusema kuwa mfumuko wa bei nchini Tanzania ni wa kiwango cha chini zaidi ikilinganishwa na nchi jirani ambapo Tanzania mfumuko wa bei kwa mwezi November ni asilimia 4.9, Kenya asilimia 7.38, Uganda asilimia 10.6 na Rwanda asilimia 21.7.
Bei ya mahindi kwa mwezi December ni kati ya Shilingi 750 na 1,890 kwa kilo, bei ya chini na ya juu imepanda kutoka 700 na 1500 kwa kulinganisha na mwezi November, Mikoa yenye bei ya juu ni Kilimanjaro, Mara na Kigoma na bei ya chini ipo katika Mikoa ya Iringa, Njombe, Songwe na Ruvuma.
Bei ya unga wa mahindi kwa mwezi Desemba ni kati ya Shilingi 1,200 na 2,050 kwa kilo, bei ya chini ya unga wa mahindi imepanda kutoka 1,000 ukilinganisha na mwezi November, bei ya chini ipo katika Mkoa wa Iringa na bei ya juu ipo katika Mikoa ya Mara, Kigoma na Kagera.