Huku ulimwengu ukiwa unajiandaa kushuhudia pambano la kukata na shoka kati ya mabondia wawili Manny Pacquiao na Floyd Mayweather linalotarajiwa kuanyika siku kumi zijazo, imefahamika kuwa mkataba wa pambano hilo bado haujatiwa saini.
Wakati Mabondia hao wakiwa kwenye maandalizi ya mwisho ya pambano hili kubwa linalosubiriwa na wapenzi wa masumbwi na hata wale wasio na upenzi na mchezo huu, promota wa Manny Pacquiao ambaye anaitwa Bob Arum amethibitisha kuwa mikataba ya pambano hilo bado haijatiwa saini na pande mbili zinazohusika.
Tiketi za pambano hili bado hazijaingia sokoni na Arum amesema kuwa sehemu ya mkataba ambao alipewa mwezi huu haikuwa kama yaliyvyokuwa makubaliano yao na upande wa Mayweather Promotions pamoja na kampuni ya MGM.
Hata hivyo taarifa hizi zimekanushwa vikali na upande wa Mayweather Promotions ambapo mkurugenzi wake Leonard Ellerbe amesema kuwa kinachomtatiza Arum ni kipengele cha mkataba ambacho kinamzuia kutokuwa na haki za kusimamia kila kitu kwneye pambano hili.
Mkurugenzi huyo wa Mayweather Promotions amekwenda mbali zaidi na kumtuhumu Bob Arum kwa kusema kuwa amekuwa akipanga njama na mawakili wake za kubadilisha baadhi ya vipengele vya mkataba wa pambano hilo na akathibiisha kuwa kila kitu kuhusu pambano hili kinaendelea kama ilivyopangwa.
Manny Pacquaio na Floyd Mayweather watapanda ulingoni Mwezi Mei tarehe mbili katika pambano linalosubiriwa kwa hamu huku kila upande ukiwa unajitamba kushinda.
Moja kati ya vitu vinavyoongeza ladha ya pambano hili ni rekodi ya kutopigwa ya Floyd Mayweather ambaye wengi wanaamini ana nafasi kubwa ya kupoteza mchezo huo kutokana na ubora wa Manny Pacquiao.