Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, ametajwa kuongoza katika kundi la wanasiasa wenye uwezo wa kuondoa changamoto zinazoikabili sekta za elimu, afya na maji.
Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Maendeleo ya Elimu (TEDRO) iliyozinduliwa jijini Dar es Salaam jana.
Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Jacob Kateri, alisema katika uzinduzi wa ripoti hiyo jana Lowasa alipata asilimia 26 baada ya watu 1,200 katika mikoa sita ya Tanzania Bara kuhojiwa.
Wanasiasa wengine waliotajwa katika ripoti hiyo kwamba, wana uwezo wa kusimamia sekta hizo na alama zao kwenye mabano ni Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba (23%), Dk. Willibroad Slaa (22%), ProF.a Ibrahim Lipumba (7%), Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli (6%) na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (5%).
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya (4%), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe (3%) na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirikia, Stephen Wasira (1.8%).
Alisema lengo la utafiti huo ni kuangalia jinsi sekta ya elimu inavyoweza kuinuka kwa kuzihusisha na sekta nyingine za afya na maji.
Alitaja mikoa na wilaya, ambako utafiti huo ulifanyika kuwa ni Dar es Salaam (Temeke), Pwani (Wilaya Kibaha Mjini), Dodoma (Bahi na Chamwino), Manyara (Mbulu na Babati Mjini), Ruvuma (Songea Mjini, Namtumbo) na Tabora (Nzega na Tabora Mjini).
NIPASHE
Fomu za kuomba kugombea nafasi mbalimbali, ikiwamo udiwani, ubunge, uwakilishi na urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), zitaanza kutolewa Jumatatu ijayo.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalim, alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana na kusema gharama ya kuchukua fomu ya kuomba kuwania urais kupitia chama hicho katika uchaguzi huo, itatolewa kwa Sh. milioni moja.
Alisema gharama ya kuchukua fomu ya kuomba kugombea ubunge wa jimbo na viti maalumu na uwakilishi itakuwa Sh. 250,000 na kwamba, fomu ya kuomba kuwania udiwani wa kata na wa viti maalumu itatolewa kwa Sh. 50,000.
Mwalim alisema fomu za kuomba kugombea ubunge zitachukuliwa katika eneo lolote la ngazi ya taifa, mkoa, wilaya na kwamba za udiwani zitachukuliwa kwenye ngazi ya wilaya, jimbo na kata.
Alisema fomu hizo pia zitapatikana mitandaoni kupitia website ya chama; www.chadema.or.tz na kwamba, zitarejeshwa kwenye jimbo au kata, ambayo mgombea anagombea, ambako ndiko atapaswa kulipia gharama za fomu husika.
Kwa upande wa ubunge wa viti maalumu, alisema fomu zao zitalipiwa moja kwa moja kwenye akaunti ya Baraza la Wanawake wa Chadema (BAWACHA) taifa, ambayo ipo kwenye fomu husika na kwamba, wagombea wa nafasi hiyo watalazimika kuambatanisha fomu zao na stakabadhi ya kibenki, ambayo inaonyesha kuwa wamelipia fomu hizo.
Mwalim alisema mchakato wa uteuzi wa wagombea utahusisha hatua tatu katika ngazi ya kata na jimbo/wilaya husika na hatua moja katika ngazi ya kitaifa.
NIPASHE
Rais Jakaya Kikwete ametoa maagizo magumu kwa viongozi wa Halmashauri ya Jijini la Dar es Salaam kwa kuwataka kuzibomoa nyumba zote zilizojengwa katika kingo za mifereji, mito na mikondo ya kupitishia maji.
Alitoa agizo hilo jana, baada ya kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko yaliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha ya Boko, Basihaya Tegeta na Mkwajuni katika wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Nyumba za wakazi wake zimezingirwa na maji kutokana na baadhi ya watu kujenga katika mifereji ya kupitisha maji na mabondeni.
Rais Kikwete akiwa eneo la Boko alimuuliza Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda na Mhandisi wa Manispaa hiyo, Baraka Mkuya, sababu za maji kujaa katika nyumba za watu na hatua zilizochukuliwa kuyaondoa.
Makonda alijibu kuwa, Manispaa ya Kinondoni imeandaa bajeti ya Sh. bilioni 3.5 ili kuondoa maji hayo pamoja na kutengeneza miundombinu.
Mkuu huyo wa wilaya alieeza sababu za kujaa maji katika nyumba kuwa imesababishwa na baadhi ya watu kujenga nyumba zao juu ya mifereji na mikondo ya kupitishia maji yanayoelekea baharini.
“Mkuu wa wilaya na watendaji wako hapa kama mnajua sababu ni watu kujenga juu ya mitaro bomoeni nyumba zote msitake kumridhisha kila mtu hamtaweza na hata mtakaowaridhisha hawatawashukuru,” Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema wale ambao hawataki nyumba zao zisibomolewe licha ya kujengwa juu ya mifereji watakuwa ni wajinga kwani hata katika nyumba hizo hawawezi kuishi kutokana na kujaa maji.
Aidha, alimwagiza mkuu huyo wa wilaya na wataalamu wake kutumia pampu 27 za manispaa hiyo kunyonya maji kutoka katika nyumba ambazo maji yamejaa badala ya kufikiria kuandaa miradi ya fedha nyingi.
Rais Kikwete aliagiza manispaa hiyo kukaa chini na watendaji wake ili kupata jawabu la kumaliza tatizo la kujaa maji katika nyumba za watu, vinginevyo maeneo hayo yatageuka kama maeneo ya kufugia samaki.
“Mhandisi hivi hauna maarifa, kwanini mmefikiria kuandaa fedha nyingi za kutengeneza miundombinu badala ya kuangalia namna ya kuondoa maji katika nyumba za watu, tumia maarifa yangu niliyoelekeza, achana na hayo ya kwako ambayo hayasaidii kumaliza tatizo kwa muda mfupi,” alisema.
Akiwa ofisi za Kampuni ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO), Rais Kikwete, alihoji sababu za maji kujaa katika ofisi hizo wakati kuna wataalamu wa maji ambao wanaweza kumaliza tatizo hilo.
Hata hivyo, Mhandisi Maro Wambura alimweleza Rais kuwa maji hayo yanatoka kwenye kiwanda cha saruji cha Wazo ambayo yanatakiwa kuelekea baharini, lakini yamekuwa yakikwama kwenye ofisi hizo kutokana na baadhi ya watu kujenga katika mikondo ya kupitishia maji.
Wambura alisema kutokana na tatizo hilo ambalo linajitokeza kila mwaka kila unapofika msimu wa mvua, wanalazimika kufunga ofisi na kwamba hawana uwezo wa kuyaondoa bila kushirikiana na manispaa.
Makonda alisema kutokanana na hali hiyo, kaya 102 zilipewa viwanja eneo la Mabwepande ili wahame bondeni, lakini kaya 42 kati ya hizo zimeshikilia maeneo Mambwepande na Mkwajuni.
Rais Kikwete aliagiza viongozi wa wilaya hiyo kuhakikisha watu wote waliojenga nyumba zao bondeni Mkwajuni wanahamishwa kwani suala la kuzuia mvua lipo nje ya uwezo wa serikali.
MWANANCHI
Hali bado si shwari Burundi. Vituo vitano vya redio ikiwamo ya Taifa na ile ya African Public Radio (RPA) kilichokuwa kimefungwa na Serikali ya Burundi vilishambuliwa jana huku kukiwa kukiwa hakuna taarifa za uhakika za nani anayeitawala nchi hiyo kwa sasa.
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Meja Jenerali Godefroid Niyombare kutangaza kumpindua Rais Pierre Nkurunziza wakati akiwa Tanzania katika kikao cha kutafuta suluhu ya mgogoro wa kikatiba wa Burundi.
RPA ilipigwa kombora la roketi ikielezwa kuwa askari wanaomtii Rais Nkurunziza ndiyo waliotekeleza shambulizi hilo.
Kituo hicho cha RPA kilifungwa na Serikali baada ya kuanza harakati za kumpinga Nkurunziza lakini kilianza kurusha matangazo yake juzi na usiku wa kuamkia jana kikapigwa kombora hilo.
Mbali na kituo hicho, vituo vya redio vilivyolipuliwa vinaelezwa kufanya harakati za kuipinga Serikali.
Vituo hivyo vilishambuliwa usiku wa kuamkia jana muda mfupi baada ya waandamanaji kuvamia kituo cha redio na televisheni ya Rema, vinavyohusishwa na chama tawala.
“Tunalaani mashambulizi kwa vyombo vya habari inatakiwa waandishi waachwe wafanye kazi zao,” alisema Mwenyekiti wa Umoja wa Waandishi wa Habari Burundi, Alexandre Niyungeko.
Alisema hakufahamu hasa ni nani aliyeshambulia vituo hivyo na kwamba yamefanyika wakati jeshi liliahidi ulinzi katika maeneo mbalimbali.
Hata hivyo, taarifa zilizochapishwa na Gazeti la Jeune Afrique zilisema vituo vya redio vilivyolipuliwa ni vitano, viwili vikilipuliwa na polisi, kimoja na waasi wanaomuunga mkono Jenerali Niyomare na viwili vikichomwa na waandamaji.
Rais Nkurunziza alituma ujumbe kwenye mtandao wa Twitter akiwataka wananchi wake kutulia kwa kuwa jeshi limezima majaribio yote ya mapinduzi.
Hata hivyo, Rais Nkurunziza ameendelea kubaki Dar es Salaam hasa baada ya kutangazwa kufungwa kwa mipaka ukiwamo Uwanja wa Ndege wa Bujumbura.
MWANANCHI
Mwanasiasa mkongwe nchini, Hamad Rashid Mohamed, atavaana na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad katika kinyang’anyiro cha urais visiwani Zanzibar.
Hamad Rashid amekuwa mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CUF kwa takriban miaka 20 sasa, lakini katika siku za hivi karibuni, alikwaruzana na chama hicho cha upinzani na kufukuzwa uanachama. Hata hivyo, alibakiwa na ubunge wake kutokana na amri ya Mahakama.
Katika mgogoro huo, Hamad Rashid alimtuhumu Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa chama hicho kuwa alifanya makusudi kuvunja amri ya Mahakama iliyomtaka asitishe kikao kilichokuwa kikijadili hatima yake ndani ya chama hicho.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, anatajwa kuwa ndiye atakayekuwa chaguo la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa nafasi ya urais Zanzibar kutokana na CUF kuwa tayari imeshaota mizizi visiwani humo.
Hiyo itakuwa mara ya tano kwa Maalim Seif kugombea urais Zanzibar kama ataingia kwenye kinyang’anyiro hicho. Alianza kugombea nafasi hiyo mwaka 1995, akagombea tena 2000, kisha 2005 na mwaka 2010 na mara zote hizo, amekuwa akishindwa kwa tofauti ya kura chache na wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Doyo Hassan alisema jana kuwa kutokana na mgogoro uliopo na hasa Ukawa kuwa tayari wameshagawana majimbo, chama hicho kitasimamisha wagombea wake na Hamad Rashid ameshajitokeza kuutaka urais Zanzibar.
Alisema Hamad Rashid ameonyesha nia yake hiyo kwa viongozi wa chama na sasa anasubiri muda wa kuchukua fomu ili aanze mchakato huo wa kuitafuta Ikulu ya Zanzibar.
“(Hamad Rashid) anasubiri muda tu aje kuchukua fomu, lakini tayari amekuja tumezungumza naye na amekubali kuja kugombea urais kupitia chama chetu,” Doyo.
Hata hivyo, Doyo alitoa wito kwa wanachama wengine wa chama hicho kujitokeza kwa ajili ya kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi pamoja na nafasi za ubunge ili kuleta ushindani utakaokiwezesha chama kuwapata wagombea bora zaidi.
“Uchaguzi ndani ya chama kwa ajili ya kumpata mgombea urais, unatarajiwa kufanyika mara baada ya watia nia kurudisha fomu mwishoni mwa Julai na mgombea wetu atajulikana mwanzoni mwa Agosti,” Doyo.
MTANZANIA
Mbunge wa Kahama Mjini, James Lembeli (CCM), ameaungana na Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba, baada ya kuzungumzia ripoti ya Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue iliyowasafisha baadhi ya watendaji serikalini waliohusika katika kashfa ya Escrow na Operesheni Tokomeza.
Akichangia bungeni jana, Lembeli alisema wakati Serikali imewasafisha baadhi ya watendaji, haoni jitihada kama hizo za kumsafisha Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa aliyejiuzulu uwaziri mkuu kutokana na kashfa ya Richmond.
Lembeli alikuwa akichangia Hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyoiwasilisha bungeni juzi akiomba Sh trilioni 5 kwa mwaka wa fedha wa 2015/2016.
Lembeli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maliasili, Utalii na Mazingira, alishangazwa na taarifa hiyo iliyowasafisha baadhi ya watu waliohusishwa katika kashfa hiyo na kuwaacha wengine, jambo ambalo alisema halitoi taswira ya usawa.
Katika mchango wake, Lembeli alisema haoni mantiki kwa Serikali kumsafisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliackim Maswi na Waziri Profesa Sospeter Muhongo na kuwaacha wengine.
Katika mchango wake juzi Serukamba alijikita zaidi katika kashfa ya Escrow wakati Lembeli alijikita katika kashfa ya Operesheni Tokomeza.
Mapema mwezi huu, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue, alisema uchunguzi dhidi ya Profesa Muhongo na Maswi, umebaini kuwa viongozi hao hawakukiuka maadili yoyote katika suala hilo.
Mbali na viongozi hao, uchunguzi mwingine wa malalamiko ya utekelezaji wa Operesheni Tokomeza uliosababisha waliokuwa mawaziri watatu kujiuzulu, pia umebaini mawaziri hao hawakujihusisha moja kwa moja na upungufu wa operesheni hiyo.
Viongozi hao ni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi na aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. David Mathayo David.
Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha.
MTANZANIA
Dalali wa Mahakama, MEM Auctioneers and General Brokers Ltd, jana alikamata na kuondoa mali za Hospitali ya African Medical Investment Ltd (AMI) maarufu kama Trauma Centre iliyoko Msasani Dar es Salaam, kutokana na kudaiwa kodi ya pango ya zaidi ya Sh bilioni tatu.
Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo mwakilishi wa kampuni hiyo ya udalali, Elieza Mbwambo, alisema kiasi hicho ni kodi ya pango ya zaidi ya miezi 26 kinachodaiwa na mmiliki wa jengo hilo, Navtej Singh Bains.
“Hapa tunatekeleza amri ya Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara ya Aprili 24 mwaka huu iliyoamuru kukamatwa kwa fedha, magari na mali za AMI ili kupigwa mnada kwa ajili ya kulipa deni la kodi ya pango na kisha kuondolewa kwenye jengo na kumkabidhi mmiliki, ”Mbwambo.
Alitaja mali zilizokamatwa kuwa ni magari matatu ya kubebea wagonjwa (ambulance), vitanda maalum vya kulaza na kuwahudumia wagonjwa, gari ndogo ya Mark II, mashine mbalimbali kama kompyuta, viti, meza, makochi na hata vitambaa na mashuka ya hospitali hiyo.
Alisema mdai aliwaomba wakamate na kuchukua vitu ambavyo havitumiki kutibu wagonjwa kwa sasa ili wagonjwa hao wahamishwe na kufikia Mei 22, mwaka huu hospitali hiyo itafungwa rasmi.
“Ingawa mahakama ilitoa amri ya kukamatwa mali zote baada ya kikomo cha notisi ya siku 14 ambayo imeisha jana, mdai amefanya ubinadamu na ametuomba kama madalali wa mahakama, kuondoa na kukamata vitu ambavyo havitumiki na wagonjwa waliolazwa.
“Tumewapa notisi nyingine ya kuwahamisha wagonjwa na hawatapokea wagonjwa wapya hadi Mai 22 mwaka huu, kisha tutaondoa kila kitu na kumkabidhi mmiliki jengo lake,” Mbwambo.
Alitaja mashine ambazo zimeachwa kwa ajili ya kuwapa huduma wagonjwa kuwa ni City-Scan, X-ray na mashine nyingine ambazo ni muhumu katika kuchunguza maendeleo ya afya ya mgonjwa.
Taarifa zaidi zinasema kwamba akaunti za Benki za Hospitali hiyo ya AMI katika Benki ya EXIM zilizoambatanishwa na Mahakama zilikutwa zimefungwa na fedha zote zikiwa zimetolewa.
Hata hivyo jana wakati wa ukamataji wa mali hizo wafanyakazi wa hospitali hiyo walionekana kupigwa na butwaa na walipohojiwa kuhusu tukio hilo walikataa kuzungumza kwa kudai kuwa wamechanganyikiwa.
“Naomba uniache siwezi kuzungumza kwa sababu nimechanganyikiwa,” alisema muhudumu mmoja aliyekuwa amevalia mavazi ya rangi ya kijani ambaye hakutaja jina lake.
Baadhi ya ndugu na jamaa wa wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo walionekana wakifanya taratibu za kuanza kuwahamisha wagonjwa wao, huku uongozi wa hosipitali ukionekana kupigwa butwaa.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa hosipitali hiyo, Lawrence Ochola alisema kwa ufupi kuwa bado madaktari wanaendelea kuwahudumia wagonjwa waliolazwa na kwamba hawezi akazungumzia zaidi suala hilo.
Amri ya kufungwa AMI ilitolewa Mei 7 mwaka huu na kusainiwa na Makamu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
HABARILEO
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ameaga rasmi katika wizara hiyo na kujivunia kuweza kuwarudisha nchini maofisa na mabalozi wote waliostaafu nje ya nchi huku akiahidi kujaza nafasi za walioshika nafasi hizo kabla hajaondoka katika wizara hiyo.
Alisema hatua hiyo imewezeshwa baada ya wizara yake kupatiwa Sh bilioni 3.3 kwani kuna walioteuliwa miaka saba hadi nane, lakini hawajaenda katika vituo vya kazi kutokana na uhaba wa fedha, ambao ni mabalozi watano na maofisa 19.
Akizungumza katika mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa wizara hiyo, Membe alisema pia watafanya mkutano wa mabalozi hivi karibuni baada ya kuwa kwa sasa wana uwezo wa kufanya kikao hicho, kwani walishindwa kufanya hivyo kwa muda mrefu.
Akiwaaga wafanyakazi hao, alisema kuwa kikao hicho ni cha mwisho, kwani kitakachokuja hatakuwa Waziri wa Mambo ya Nje na atakapokuwa ni siri ya Mungu, kwani atajaribu vitu vingine.
“Haitawezekana wala kutokea tena kuwa waziri wa mambo ya nje, lakini kwa jinsi wizara hii inavyopika viongozi, kwani asilimia 40 ya wafanyakazi wa Ikulu ni kutoka wizara hii, nikipata ajira popote nitaajiri kutoka wizara hii, kinachotakiwa ni kuombeana,” .
Membe alisisitiza kuwa hakuna wizara inayotoa viongozi mbalimbali kama hiyo, kwani inapika viongozi, siyo wa diplomasia ya siasa na uchumi tu, bali viongozi wengine wa kada mbalimbali.
Alisema pamoja na matatizo ya kifedha waliyonayo katika wizara hiyo, wameweza kuzalisha viongozi wazuri akiwemo yeye, ambaye anatokea kwenye wizara hiyo, ambapo alisema wameongeza posho kwa wafanyakazi wa wizara hiyo wanaofanya kazi wakati wa ziada.
HABARILEO
Mwanamke mwenye ulemavu wa ngozi (albino), Remi Luchoma (30), mkazi wa kijiji cha Mwamachoma kata ya Mamba wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi, amekatwa mkono wake wa kulia na watu wasiojulikana, kisha wakatokomea na kiganja cha mkono huo kusikojulikana.
Kwa sasa, mtu huyo amelazwa katika Hospitali ya wilaya ya Mpanda kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Mpanda, Dk Joseph Mkemwa alithibitisha kumpokea mama huyo na kwamba anapatiwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri.
Alieleza kuwa tukio la kukatwa mkono wa albino huyo, lilitokea hapo jana majira ya saa 6 usiku nyumbani kwa wazazi wake katika kijiji hicho.
Alisema baada ya kukatwa kiganja chake cha mkono wa kulia, albino huyo alipelekwa katika Kituo cha Afya cha Mamba, ambapo alipewa rufaa na kukimbizwa katika Hospitali ya wilaya ya Mpanda kwa ajili ya matibabu zaidi.
Alipokewa katika hospitali hiyo ya wilaya saa 10 alfajiri na amelazwa wadi namba mbili .Hali yake inaendelea vizuri.
Kwa upande wake, Masuma Luchuma ambaye ni kaka wa albino huyo, alisema tukio hilo la dada yake kukatwa kiganja cha mkono ni la kinyama na limemsikitisha.
Alisema tukio hilo lilitokea kwenye chumba alichokuwa akiishi albino huyo, mwenye watoto wanne.
Kaka huyo alisema siku ya tukio majira ya saa 6 usiku, alisikia watu wakivunja mlango wa chumba alichokuwa amelala Remi na baada ya muda mfupi, alisikia dada yake huyo akipiga mayowe ya kuomba msaada.
Alidai alijaribu kutoka nje ili kumwokoa dada yake huyo, lakini alishindwa kutoka nje kwa kuwa watu hao walifunga mlango wake kwa nje. Alisema hali ya kufungiwa ndani, ilimfanya apige kengele ya jembe, kama ishara ya kuomba msada kwa majirani .
Hali hiyo iliwafanya watu hao, wakimbie na kutokomea kusikojulikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahri Kidavashari alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanaendelea na msako mkali kuwasaka waliohusika na tukio hilo.
HABARILEO
Serikali imehadharishwa kutowatenga Watanzania na ulimwengu kwa kutekeleza sehemu ya Sera ya Elimu, inayotaka Kiswahili kiwe lugha ya kufundishia kutoka shule ya awali mpaka chuo kikuu.
Mbunge wa Urambo Magharibi, Prof. Juma Kapuya, ametoa hadhari hiyo bungeni jana wakati alipokuwa akichangia katika mjadala wa makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu unaoendelea.
Profesa Kapuya alikumbusha maoni ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliposema kuwa Ki ingereza ndio Kiswahili cha dunia. Profesa Kapuya amewahi kuwa waziri wa elimu na mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Alionya kuwa Watanzania watafanya kosa kubwa litakalowagharimu katika Jumuiya za kikanda hasa katika ushindani wa ajira, kama wataondoa Kiingereza kuwa lugha ya kufundishia.
Alitoa mfano wa nchi ya Rwanda, ambayo imebadilisha lugha ya kufundishia kutoka Kifaransa kwenda Kiingereza na kuongeza; “Nenda pale Rwanda uone mtoto wa darasa la saba anavyozungumza Kiingereza kizuri.”
Aliwajia juu wanaoshabikia Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia kutoka shule ya awali mpaka chuo kikuu, kwamba ni wanafiki kwa kuwa wenyewe watoto wao wamewapeleka katika shule za mchepuo wa Kiingereza.
Alisema watua hao wamekuwa wakitoa mfano wa China na Japan, lakini wanasahau kuwa nchi hizo zina historia tofauti ya elimu ikilinganishwa na nchi za Afrika hususani Tanzania.
“Kule Afrika Kusini wakati wa mauaji ya Soweto, moja ya madai ya Waafrika Kusini ni kuacha kufundishwa kwa kutumia lugha ya Afrikaans na Kizulu, na badala yake wafundishwe kwa Kiingereza ili wawe sehemu ya ulimwengu,” Prof. Kapuya.
Alionya kuwa kama Serikali itaendelea na mpango huo wa kutekeleza sehemu ya Sera ya Elimu ili Kiswahili kiwe lugha ya kufundishia, hatari ya kwanza itakuwa kulazimisha baadhi ya watu kujifungia na kuanza kutafsiri mawazo ya watu.
Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyezahapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahaukusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video yaAyoTVikufikie.