Upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mkurugenzi wa Tathmini, Archard Alphonce Kalugendo mwenye umri wa miaka 49 na Mthamini wa Madini ya Almas wa Serikali, Edward Joseph Rweyemamu mwenye umri wa miaka 50, leo October 12, 2017 umeileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa, sehemu kubwa ya upelelezi umekamilika bado maeneo machache.
Wakili wa Serikali, Wankyo Simon amemueleza Hakimu Mwandamizi, Godfrey Mwambapa kuwa kesi hiyo imeitishwa kwa ajili ya kutajwa.
Wakili Wankyo amedai wanakamilisha upelelezi katika sehemu ndogo iliyobakia na wamewaelekeza Polisi kufanya hilo na kwamba tarehe ijayo wataieleza Mahakama hatua ya upelelezi ilipofikia
Hakimu Mwambapa ameahirisha kesi hiyo hadi October 26, 2017 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa
Washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kusababisha hasara ya Dola za Kimarekani 1,118,291.43 sawa na Tsh 2,486,397,982.54.
Kalugendo ambaye ni Mkazi wa Kinyerezi na Rweyemamu Mkazi wa Mwananyamala wote ni waajiriwa wa Wizara ya Nishati na Madini abapo wanadaiwa kati ya August 25 na 31, mwaka huu, katika maeneo mbalimbali kati ya Dar es Salaam na Shinyanga, kwa pamoja na kwa vitendo vyao wakiwa wathamini walioajiliwa na Wizara ya Nishati na Madini walisababisha hasara ya kiasi hicho cha fedha.
Rais JPM: “Kama Aga Khan imesamehewa kodi, mbona gharama za huduma bado ziko juu?”