Mchezaji wa soka wa timu ya taifa ya Ufaransa, Nicolas Anelka, anayeichezea klabu ya Westbrom amekanusha madai ya kufanya ishara inayoaminika kuwa ya kibaguzi dhidi ya Wayahudi.
Anelka amesema atapinga vikali mashtaka dhidi yake ambayo huenda yakasababisha kupigwa marufuku ya kutoshiriki katika mechi yoyote ya soka ikiwa atapatikana na hatia.
Anelka, mwenye umri wa miaka 34, ameshutumiwa vikali kwa kufanya ishara hiyo, ambayo ilipigiwa debe sana na msanii wa Ufaransa Diedonne M’bala M’bala, ishara ambayo ilitajwa na wakosoaji kuwa ishara ya utawala wa Kinazi.
Mshambuliaji huyo wa Westbrom, amesema atapinga mashtaka hayo yaliyowasilishwa na chama cha mchezo wa soka nchini Uingereza.
Ikiwa atapatikana na hatia Anelka huenda akakabidhiwa adhabu ya kutoshirika katika mechi tano mfululizo.
Klabu ya Westbrom halijasema lolote kuhusiana na mashtaka hayo ya FA, lakini imekariri kuwa Anelka ataendelea kuichezea klabu hiyo hadi kesi hiyo itakapoamuliwa.