SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema changamoto kubwa linaloikabili sasa ni madeni ya mamilioni ya fedha waliyoyarithi kutoka uongozi uliopita wa Rais, Leodegar Tenga.
Akizungumza na Mwanaspoti katika tathimini yake ya siku 100 tangu alipochaguliwa kuwa rais mpya wa shirikisho hilo, Jamal Malinzi, alisema madeni hayo ni makubwa ukilinganisha na kipato cha TFF kinachotegemea zaidi mapato ya milangoni ya mechi mbalimbali.
“Madeni tuliyoyakuta ni makubwa, lakini mengine tumegundua ni hewa, hivyo yanafanyiwa uhakiki ili tujue madeni halisi ili tuweze kuyalipa,” alisema Malinzi aliyeingia madarakani Oktoba 27, mwaka jana.
“Pia tunafanya mazungumzo na watu wanaoidai TFF ili watupe masharti nafuu ya kulipa madeni hayo.”
Kauli ya Malinzi imekuja ikiwa imepita miezi sita tangu TFF ipate aibu ya mabasi yake kukamatwa na Kampuni ya Udalali ya Flamingo ili kufidia deni la zaidi ya Sh50 milioni.