Taasisi ya Wanawake Wahasibu Tanzania (TAWCA) wametoa msaada wa vitabu mbalimbali vya hesabu na masomo ya biashara vyenye thamani ya Milioni 8.5 kwa Shule ya Sekondari Turiani jijini DSM.
Uamuzi wa TAWCA kutoa msaada huo kwenye shule hiyo ni kuwahamasisha wanafunzi hasa wa kike kupenda masomo ya hesabu nchini ili baadae waje kuongeza idadi ya watalaamu wahasibu nchini.
Akizungumza shuleni hapo wakati wa tukio la kukabidhi msaada huo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Wanawake Wahasibu Tanzania, Tumaini Lawrence amesema wanawake wahasibu nchini wameona haja ya kushiriki kwa vitendo kuhamasisha wanafunzi kusoma masomo yanayohosu hesabu na ndio maana wameamua kutoa msaada huo wenye lengo la kuwahamasisha wanafunzi wa kike nchini kupenda hesabu.
“Wanawake wahasibu nchini kwa umoja wetu tumeamua kuchangishana fedha ili kufanikisha msaada huu kwa ajili ya wanafunzi wa Sekondari ya Turiani” Lawrence
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya taasisi hiyo Neema Msusa amesema ni faraja kwao kufika shuleni hapo kuzungumza na wanafunzi hao.
“Tumefika shuleni hapa kwa lengo la kumsha ari kwa wanafunzi wetu wa kike kusoma masomo ya biashara. Tunawaambia hesabu haikimbiliki, hivyo wasome kwa bidii kwani tunaona faida ya kusoma hesabu maana wanawake wahasibu kila mmoja yupo kwenye taasisi anafanya kazi yake vizuri,” Msusa
Ameongeza wao kuwa wahasibu kumetokana na msingi mzuri ambao uliwekwa na walimu wao kuanzia ngazi ya chini , hivyo wanaamini wanafunzi wa kike watasoma kwa bidi masomo ya hesabu.