DAKTARI Mkuu wa Simba, Yassin Gembe, amezuia beki wake wa kati raia wa Burundi, Gilbert Kaze, kucheza mechi tano za Ligi Kuu Bara walizobakiwa nazo kwenye msimu huu.
Uamuzi wa daktari huyo unalenga kumpa Kaze muda wa kupona maumivu ya goti yanayomwandama. Beki huyo alisajiliwa Msimbazi baada ya ushawishi mkubwa wa straika, Amissi Tambwe.
Beki huyo alipata maumivu hayo akiwa mazoezini na kwa mujibu wa Dk. Gembe, Kaze anatakiwa kuwa nje ya uwanja kwa wiki tatu.
Dk. Gembe alisema beki huyo ameanza kupata nafuu na ameanza mazoezi ya binafsi ya ufukweni kabla ya kujiunga na programu nyingine na wenzake ndani ya uwanja.
Hata hivyo alisema hataweza kucheza mechi tano muhimu ambazo ni ngumu dhidi ya Azam FC, Yanga, Coastal Union, Ashanti na Kagera Sugar.
“Kaze anaweza kucheza kiasi, lakini ugumu unakuja kwani mechi tano tulizozibakiza zote ni ngumu, kama atacheza huenda akajitonesha na kusababisha kuanza upya matibabu,’ alisema na kusema atasuburi msimu ujao.