Rais Magufuli amepokea gawio la Serikali la shilingi Bilioni 2.1 kutoka Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) baada ya Shirika hilo kupata faida ya shilingi Bilioni 8.3 katika kipindi cha mwaka 2018/19.
Akizungumza baada ya kupokea mfano wa hundi ya gawio la shilingi Bilioni 2.1, Rais Magufuli ameipongeza TTCL kwa hatua kubwa ilizopiga katika kipindi kifupi na ameeleza kuwa kabla ya kuanza kutoa gawio mwaka jana shirika hilo lilikuwa likipata hasara ya shilingi Bilioni 15 kila mwaka kwa kipindi cha miaka 15 jambo ambalo halikubaliki.
Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na juhudi za TTCL kuongeza wateja kutoka Milioni 1.8 mwaka jana hadi kufikia Milioni 2.2, kuanzisha kampuni ya huduma za kifedha ya T-Pesa yenye wateja 400,000, mawakala 14,000 na mtaji wa shilingi Bilioni 6 na kuanzisha huduma ya kuhakiki pembejeo za wakulima.
Rais Magufuli ameagiza fedha za ruzuku ambazo hutolewa na Serikali kwa Mfuko wa Mawasiliano kwa kampuni zote za simu kwa ajili ya kujenga minara katika maeneo yasiyokuwa na huduma za mawasiliano zielekezwe kwa TTCL pekee ili shirika hilo la umma lijenge minara yake badala ya kukodi kutoka kwa kampuni binafsi ambako hulipa kati ya shilingi Milioni 700 na Milioni 800 kila mwezi.
Pia, Rais Magufuli ameelezea kutofurahishwa na taasisi na viongozi wa Serikali ambao hawajaitikia wito wa kutumia huduma za mawasiliano za TTCL na amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Bw. Waziri Kindamba kumpelekea orodha ya Mawaziri wanaotumia simu za TTCL.
Kuhusu utoaji wa gawio la Serikali, Rais Magufuli amemuagiza Msajili wa Hazina kuhakikisha taasisi zote zinazopaswa kutoa gawio la Serikali zinafanya hivyo vinginevyo zifutwe.
RAIS MAGUFULI ALIVYOMHOJI MKUU WA MKOA KWA NJIA VIDEO “VIPI SUALA LA TUNDUMA”