STRAIKA namba moja wa Simba, Amissi Tambwe ametoa ya moyoni baada ya kutamka hadharani kwamba anatamani angekuwa anacheza na mawinga wenye kasi na ubora kama wa Yanga kwani makipa na mabeki wangemtambua.
Tambwe ambaye ni raia wa Burundi amesisitiza kwamba angekuwa na wachezaji hao mpaka sasa angekuwa amepachika mabao mengi na kazi yake ingekuwa rahisi zaidi tofauti na sasa ambapo amekuwa akitumia nguvu nyingi zaidi Simba kutokana na aina ya uchezeshaji.
Yanga mara nyingi inawachezesha mawinga wenye kasi ambao ni Simon Msuva, Hamis Kiiza na Emmanuel Okwi huku washambuliaji wa kati wakisimama Didier Kavumbagu, Mrisho Ngassa wakati mwingine Said Bahanuzi ambaye hana uhakika wa namba kikosini.
Tambwe alisisitiza licha ya upinzani wa Simba na Yanga lakini mtu akifanya kitu kizuri kiuanamichezo husifiwa, alisema kuwa mawinga wa Yanga wana uwezo mkubwa wa kupiga krosi na kutengeneza pasi nzuri za kufunga mabao.
“Ujue siku zote katika mechi zetu, mara nyingi utanikuta nipo katika eneo la 18 nikisubiria pasi na krosi kutoka kwa mawinga na viungo wenye jukumu la kunichezesha ikiwemo kunipa pasi na krosi nzuri za kufunga mabao.
“Vitu ambavyo sivipati kwa ubora unaostahili Simba, ninaamini kama timu yangu ingekuwa na mawinga wazuri kama wa Yanga wenye uwezo mkubwa wa kupiga krosi na pasi nzuri za kufunga, basi ningefunga mabao mengi hadi sasa katika Ligi Kuu.
“Kiukweli kabisa tuweke pembeni upinzani wetu, ninaipenda sana kombinesheni na aina ya uchezaji wanayoitumia Yanga ndani ya uwanja, ujue mimi kazi yangu kufunga mabao, hivyo ni lazima nipewe mipira mizuri ya kufunga,”alisema Tambwe ambaye habari za ndani zinadai kwamba baadhi ya vigogo wa Kundi la Friends of Simba wanajipanga kumtumia kama chambo kwenye kampeni za uchaguzi wa Simba mwezi ujao.
Mchezaji huyo ana mkataba wa miaka miwili na Simba, lakini wamekubaliana msimu wa kwanza ukimaliza watakaa chini kujadiliana jinsi ya kuendelea na mwaka wa pili.
Habari zinadai kwamba vigogo hao wamepanga kumlipa fedha za mkataba wa mwaka wa pili na kumhakikishia maisha mazuri Simba na watatumia upenyo huo kama sehemu ya kampeni za uchaguzi wa mwezi ujao.
SOURCE: MWANASPOTI