Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Morogoro, SP Albert Kitundu (49) ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe alikataa kuandika maelezo polisi kuhusu watu anaodai waliuliwa na Jeshi la Polisi kwenye operesheni mkoani Kigoma.
Pia amedai katika upelelezi walioufanya wakati huo akiwa Msaidizi wa Mkuu wa Upelelezi Kinondoni, alibaini kuwa kilichosemwa na Zitto hakikuwa na ukweli kwani watu waliofariki si 100 kama alivyodaiwa bali ni wanne ikiwemo Askari Polisi wawili.
Hayo yamebainishwa na SP Kitundu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati akitoa ushahidi ambapo aliongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga.
Akitoa ushahidi wake, SP Kitundu amedai kuwa Zitto alikamatwa na Maofisa wa Jeshi hilo baada ya kutoa maneno ya uchochezi, kisha kufikishwa kituo cha Polisi Oysterbay na kumuhoji kawaida.
Miongoni mwa maswali aliyomuhoji ni nafasi yake katika chama cha ACT Wazalendo, historia ya maisha yake ikiwemo elimu ambayo aliyaeleza kwa kirefu.
SP Kitundu amedai alipomuuliza kuhusu tuhuma alizozitoa kwa jeshi hilo, alikiri kufanya mkutano na waandishi wa habari na kutoa ufafanuzi kuhusu watu 100 aliodai wameuliwa.
“Baada ya kueleza hayo nilimwambia Zitto nataka kumuhoji kama mtuhumiwa ili maelezo yake yaweze kutumika kama kielelezo mahakamani. Nilimpa haki zake lakini alisema hayuko tayari kutoa maelezo yake polisi na kudai atayatoa mahakamani,” alidai SP Kitundu.
Alidai walimuomba taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari na kuwapatia.
Kuhusu upelelezi wa tuhuma hizo, shahidi huyo alidai aliongoza upelelezi wa tukio hilo kwa kupitia hobuba ya Zitto ambayo mmoja wa maofisa wa polisi aliichukua kwenye mkutano wake ambapo walikuta maneno ya kichochezi yalikuwa yanatakiwa kutolewa ufafanuzi na mshitakiwa huyo.
Alidai maneno yaliyotakiwa kutolewa ufafanuzi ni kwamba “polisi limeuwa wananchi wapatao 100 na waliokwenda kutibiwa katika Zahanati ya Nguruka, polisi walichukua majeruhi na kuwaua.”
Alidai baada ya kusikiliza maelezo hayo, alielekeza askari polisi wahakikishe wanampata Zitto ili waweze kumuhoji.
Pia alidai aliwasiliana na RCO wa Kigoma na kutaka awapatie taarifa kuhusu tuhuma zilizotolewa na Zitto ambaye aliwapa maelezo ya watu mbalimbali aliowahoji.
“Niligundua kilichosemwa hakikuwa na ukweli kwani watu wanne ndio waliopoteza maisha kati yao wawili ni askari polisi na wawili ni wananchi.
Kuhusu majeruhi hakuna aliyechukuliwa na polisi na kuuawa isipokuwa waluwachukua ili kuwahoji kuhusu operesheni iliyotokea,” alidai SP Kitundu.
Baada ya kutoa ushahidi huo, Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 22, mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa.
Katika kesi hiyo, Zitto anadaiwa Oktoba 28, 2018 Zitto akiwa katika mkutano na waandishi wa habari, uliyofanyika katika Makao Mkuu ya ofisi ya Chama cha ACT Wazalendo alitoa maneno ya uchochezi yenye kuleta hisia ya hofu na chuki.
Inadaiwa alisema ” Watu ambao walikuwa ni majeruhi katika tukio la mapambano baina ya wananchi na polisi wakiwa wamekwenda hospitali kupata matibabu katika kituo cha afya Nguruka, Polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali kituo cha afya Nguruka kupata matibabu wakawafuata kule wakawaua”.