Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imezitaka shule binafsi nchini, kuwapokea wanafunzi wote na kuwaruhusu waendelee na masomo pasipo ubaguzi wowote.
Agizo hilo limetolewa kufuatia uwepo wa malalamiko kutoka kwa baadhi ya wazazi juu ongezeko la ada linalofanywa na baadhi ya shule kwa kigezo cha janga la corona.
Taarifa iliyotolewa na kusainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa wizara hiyo Bi. Sylvia Lupembe, imewataka wazazi pamoja na uongozi wa shule husika kuheshimu makubaliano ya ulipaji ada yaliyokuwepo hapo awali kabla ya janga la corona na kuzingatia pia mwongozo uliotolewa na wizara mara baada ya Rais Magufuli kutangaza kuwa shule zote nchini zifunguliwe ifikapo Juni 29 mwaka huu.
Taarifa hiyo ya Wizara inasema haitakuwa busara kwa shule kutoza gharama ya usafiri iliyokuwa ilipwe wakati shule zimefungwa na badala yake watoze gharama kama vile ankara za maji, umeme pamoja na mishahara ya walimu na watumishi wengine, gharama ambazo kimsingi hazikusimama wakati wa janga la corona.
Aidha, taarifa hiyo imewataka wazazi nao kuwa waungwana kwa kuhakikisha wanalipa ada na gharama zote stahiki kwa wakati ili kuziwezesha shule nazo kuendelea kutoa elimu pasipo kikwazo chochote.