Tanzania imeruhusu nchi 15 kupitia balozi zao kuleta waangalizi wa kimataifa katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika oktoba 28 mwaka huu, baada ya balozi hizo kuwasilisha maombi na kufuata taratibu zilizowekwa.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi jijini DSM, wakati akifanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya Balozi Manfred Fanti, ambapo amesema kuwa kwa mara ya kwanza uchaguzi huo unafanyika kwa kutumia fedha za ndani na sio wahisani kama miaka iliyopita.
Mbali na Balozi wa Ulaya Prof. Kabudi pia amekutana na Balozi wa Italia Roberto Mengoni, na Balozi wa Poland ambapo amekabidhi vitabu vya sheria ,kanuni na miongozo mbalimbali inayohusu masuala ya uchaguzi ili kuwapa fursa ya kufahamu jinsi uchaguzi unavyoendeshwa.
Kwa upande wake Balozi wa Umoja wa Ulaya Manfred Fanti amesema, ameridhishwa na namna kampeni zinazofanyika kwa uhuru na amani na sasa wanajiandaa na uangalizi wa uchaguzi huo.
Naye Balozi wa Italia hapa nchini Roberto Mengoni amesema, anavutiwa na namna ambavyo vyombo vya habari vimekuwa vikitoa nafasi kwa wagombea wote bila ubaguzi na ambavyo Watanzania wanajitokeza kusikiliza sera na kudai kuwa ana imani kiongozi atakayechaguliwa atatokana na utashi wa wananchi.