Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi, amesema kuwa leo mara baada ya kufika katika anga la Chato, aliona mashimo mengi chini ikiwa ni kiashirio cha uchimbaji wa dhahabu na kusema kuwa Geita ni mkoa tajiri.
Kauli hiyo ameitoa hii leo Januari 11, 2021, wakati akizungumza na wananchi wa Chato, mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda, Chato, pamoja na mwenyeji wake Rais Dkt. John Magufuli.
“Tumeona huu mkoa ni mkoa tajiri kabisa, tumeona wameanza kuchimba chimba mashimo, wakichimba nadhani kuna dhahabu pale, tumeona mpunga na mashamba nadhani kuna samaki pia, nawapa hongera wananchi wa Geita, kitu kikubwa ni kuchapa kazi, nitaongea na Rais mpaka jioni, tutazungumzia kuhusu maendeleo ya nchi zetu”, Rais Nyusi.
Awali akimkaribisha hapa nchini, Rais Magufuli amesema kuwa, “Rafiki yangu nakushukuru sana kwa kuja Chato, Rais wa Msumbiji anafahamu Kiswahili, anayajua maisha ya Watanzania, urafiki kati ya hizi nchi mbili ni wa muda mrefu, sisi ni ndugu na ndani ya serikali tuna makubaliano ya kufanya kazi pamoja”.