Tume ya Mawasiliano ya Uganda imeamuru kampuni za mawasiliano Nchini humo kuzima internet kuanzia Jana usiku hadi watakaporuhusiwa tena, agizo hilo lilitolewa saa chache tu usiku wa kuamkia leo, kabla ya uchaguzi wa Rais kuanza.
Rais wa muda mrefu Uganda Yoweri Museveni anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa mgombea wa upinzani Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine.
Waganda wengi wameelezea kutoweza kupata huduma za Internet kwenye simu zao usiku wa kuamkia leo, Kampuni inayofuatilia masuala ya Internent NetBlocks imesema Uganda imekumbwa na ukosefu wa Internet kuanzia jana saa moja usiku.
Mkurugenzi wa kampuni ya mawasiliano MTN ya Afrika Kusini inayohudumu Uganda Nompilo Morafo amethibitisha kwamba kampuni yake pamoja na wahudumu wengine Uganda wameamriwa kuzima njia zote za Internet.
Hatua ya Uganda kuzima Internet imejiri siku moja tu baada ya Taifa hilo kutangaza pia kufungia mitandao yote ya kijamii na huduma za kutuma ujumbe mfupi kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Source idhaa ya Kiswahili