Shirikisho la Wamachinga Tanzania (SHIUMA) limeomba kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan ili wamweleze kero walizonazo.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Oktoba 20, 2021 na Makamu Mwenyekiti wa wamachinga Taifa , Steven Lusinde wakati akitoa ufafanuzi kuhusu vurugu za wamachinga zilizotokea jana katika soko la Kariakoo.
Lusinde alisema Samia ndiye Rais wa kwanza kutenga fungu la fedha kwa ajili ya maendeleo ya wamachinga na kwamba mkutano huo utamwezesha kupokea maoni kutoka kwao moja kwa moja nini fedha hizo kiasi cha Sh 5 bilioni zifanye kwa manufaa ya wajariamali hao wadogo.
“Tunamshukuru sana Rais ametoa zaidi ya Sh5 bilioni kuhakikisha yanaorodheshwa maeneo hayo kwa ajili ya wamachinga, sisi tupo pamoja na yeye akutane na sisi wamachinga wa mikoa yote tumueleze hata asiyoyajua”- Lusinde
“Yeye mwenyewe apange wapi ili tumweleze changamoto zetu na tushauri fedha hizo zinaweza kutatua changamoto zipi mengi yasiweze kutokea”- Lusinde
Amesisitiza kuwa viongozi wanatakiwa wawashirikishe machinga maeneo wanayotaka kwenda kuwaweka ili kuondoa sintofahamu.
“Watushirikishe sisi changamoto zipo,ukiangalia maeneo mengi waliyoenda bila usumbufu walitushirikisha tunaamini kila kitu kitaenda sawasawa,” amesema Lusinde.
Makamu mwenyekiti Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuph Namoto amesema viongozi wa kundi hilo wana wajibu wa kuishauri Serikali katika kufanya maboresho changamoto zilizopo katika hayo maeneo mbalimbali ili kuhakikisha wamachinga wanakuwa na mazingira bora ya biashara.
Machinga eneo la Shekilango Mohamed Shaban, amesema ameamua kubomoa banda lake kwa kufuata sheria bila shuruti hata hivyo amesema eneo analopelekwa halina biashara za uhakika ikilinganishwa na alipokuwepo.