Serikali imeahidi kuendelea kushirikiana na sekta binafsi kuinua sekta ya Kilimo na kuboresha maisha ya Wananchi wanaojishughulisha na Kilimo.
Akizungumza Jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa programu ya Africa Connect Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde amesema ili kufikia malengo ya kukuza sekta ya Kilimo hadi kwa asilimia 10% ifikapo mwaka 2030 serikali itashirikiana na kila mdau mwenye nia njema ya kuwanufaisha wakulima na Taifa kwa ujumla.
Mavunde ameongeza kuwa Serikali haitashirikiana na taasisi ambayo itaonesha dalili za kudhulumu au kuwanyonya Wakulima.
“Kabla ya kuja kushirikiana nanyi kwenye Uzinduzi wa programu hii nilitumia muda wangu kujiridhisha kama hili suala lina maslahi kwa wakulima”- Anthony Mavunde.
Mavunde amebainisha kuwa hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kuongeza bajeti ya umwagiliaji kutoka shilingi Bilioni 51 Mwaka 2021/2022 hadi Bilioni 361 Mwaka 2022/2023 ni kuelekea kwenye kuipa nchi uwezo wa kuendesha shughuli za kilimo bila kutegemea Mvua.
Program ya Africa Connect nalenga kuwasaidia wakulima wa mpunga kuweza kupata mikopo pamoja na huduma za miongozo ya uzalishi wa mpunga na hatimaye kuwaunganisha na Masoko.
Awali akizungumza kabla ya uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Yara Winstone Odhiambo amesema Yara kwa kushirikiana na wadau inatarajia kuwafikia wakulima zaidi ya 100,000 katika mikoa yote ya kilimo cha mpunga huku ikilenga kuongeza uzalishaji wa mpunga na kusaidia mpango wa Serikali wa Usalama wa Chakula.
“Huduma hii pia inalenga kuhakikisha wakulima wanafuata ubora katika hatua zote za kilimo ili wapate mazao bora, hivyo basi kutembelewa na mabwana shamba wetu waliotapaka karibu nchi nzima“- Winstone Odhiambo