Rais wa Kenya, William Ruto leo akiwa Nairobi amesema kikao chake cha jana na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa Jijini Nairobi hakijafungua tu fursa za usafiri bali kimeondoa vikwazo vingi vya kibiashara ambapo December mwaka huu nyama kutoka Kenya itaanza kuuzwa Afrika Kusini baada ya kuzuiwa kwa miaka 10.
Ruto amesema “Jana hatujafungua tu fursa za usafiri, tumeondosha vikwazo, tulikuwa tumepigwa marufuku kwa miaka 10 sasa kwa nyama ya Kenya kuingizwa kwenye soko la Afrika Kusini lakini kuanzia December mwaka huu marufuku hiyo inaondolewa na nyama kutoka Kenya itauzwa Afrika Kusini”
“Chai inayolimwa na kuzalishwa Kenya pia ilizuiwa kuingia Afrika Kusini, nimeongea na Rais Ramaphosa na tumekubaliana kuanzia January 2023 tutakuwa na uwezo wa kuingiza chai yetu kwenye soko la Afrika Kusini”
Itakumbukwa jana Rais Ramaphosa alitangaza kuwa kuanzia January 2023 Wakenya wataruhusiwa kwenda Nchini South Africa bila kuhitajika kuwa na VISA kama ilivyo sasa.