Waziri wa Nishati, January Makamba amesema kuwa hali ya miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme nchini imeendelea kuimarika na kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wateja.
Makamba ameyasema hayo tarehe 18 Januari, 2023, wakati Wizara ya Nishati ikitoa taarifa ya hali ya umeme nchini kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini jijini Dodoma.
Makamba amesema kuwa, Serikali imeendelea kutenga bajeti kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu ya Umeme na kujenga miundombinu mipya ambapo katika mwaka wa fedha 2022/23, jumla ya shilingi bilioni 711.56 zitatumika kwa kazi husika zikijumuisha shilingi bilioni 400 za kuimarisha Gridi.
“Kupitia miundombinu hiyo, TANESCO imeweza kuunganishia wateja wapya 331,034 ndani ya miezi sita kuanzia Julai, 2022 hadi Desemba, 2022 sawa na asilimia 166 ya lengo la kuunganisha wateja wapya 200,000 katika kipindi hicho.” Makamba
Amesema kuwa, kuvuka kwa lengo hilo kumetokana na kuanzishwa kwa mfumo mpya wa maombi ya umeme wa Nikonekt pamoja na utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini na kufanikisha kufikia wateja 4,173,130 ikilinganishwa na wateja 3,655,534 waliokuwepo kufikia mwezi Januari, 2022 sawa na ongezeko la asilimia 13.47.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dunstan Kitandula ameipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali inazozichukua ili kuhakikisha hali ya miundombinu ya kusambaza na kusafirisha umeme nchini inaendelea kuimarika pamoja na uzalishaji wa umeme.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mha.Innocent Luoga pamoja na watendaji wengine kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).