Mbunge wa Jimbo la Ushetu Mhe. Emmanuel Cherehani amesema mpaka sasa hatua zilizofanywa na Serikali kupitia wizara ya kilimo ya kuongeza makampuni ya ununuzi wa tumbaku itasaidia kukuza thamani ya zao hilo baada ya kukosekana kwa wanunuzi hapo awali.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme, Mhe. Cherehani amesema kuwa mbali na changamoto zinazowakabili wakulima wa Tumbaku serikali imeendelea kufanya jitihada za kuongeza thamani katika zao hilo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wakulima hao wanalipwa kwa Dola hatua inayokuza thamani ya zao la tumbaku nchini.
“Kipindi hiki cha Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Bashe wameruhusu makampuni kuingia bei na kupanda mpaka kufikia dola 3, na leo tunavyoongea thamani ya dola inazidi kuongezeka hivyo ni ongezeko kubwa la fedha ambazo zinakwenda kwa Wananchi hawa” ameeleza Mhe. Cherehani.
Itakumbukwa mara kadhaa Mhe. Cherehani amekuwa akiiomba serikali kuboresha maslahi ya wakulima wa zao la tumbaku kwa kuwawekea mazingira wezeshi ya kibiashara yatakayowanufaisha na kuwatoa katika wimbi la umasikini.