Kusimamisha vita kwa muda hakutatosha kuwakomboa mateka zaidi ya 100 ambao Israel inasema bado wako Gaza, afisa wa Hamas amesema.
Vita vya Israel na Hamas tayari vimewafurusha karibu 85% ya watu milioni 2.3 wa Gaza kutoka makwao, na kusawazisha sehemu ya kaskazini ya eneo hilo na kuzidisha hofu kuhusu hatima kama hiyo kwa upande wa kusini huku mashambulizi ya anga na ardhini ya Israel yakiongezeka.
Lakini afisa wa Hamas alisema jana “kusitishwa kwa sehemu au kwa muda kwa uchokozi” hakutatosha kuwakomboa wale wanaosalia mateka katika eneo hilo.
Zaidi ya Wapalestina 20,000, thuluthi mbili yao wakiwa wanawake na watoto, wameuawa tangu kuanza kwa vita hivyo, kwa mujibu wa wizara ya afya huko Gaza inayoendeshwa na Hamas, ambayo haitofautishi kati ya raia na wapiganaji miongoni mwa waliofariki.
Takriban watu 1,200 waliuawa baada ya Hamas kuvamia kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba, huku takriban watu 240 wakichukuliwa mateka.