Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Azam FC hii leo wamefanikiwa kurejea kwenye kilele cha ligi hiyo baada ya kuwafunga Mtibwa Sugar 5-2 katika mchezo uliopigwa huko Azam Complex, Chamazi.
Azam walifunga mabao yao kupitia kwa mshambuliaji Kipre Tchetche ambaye alifunga mabao mawili, Frank Domayo ambaye pia alifunga mawili na Didier Kavumbagu huku Mtibwa wakifunga kupitia kwa Ali Shomari na Ame Ali.
Matokeo ya mchezo huu yamewafanya Azam FC warudi kwenye kilele cha ligi hiyo wakiwa wamekusanya jumla ya pointi 25 ambapo wanawazidi Yanga kwa idadi kubwa ya mabao.
Huu unakuwa mchezo wa pili mfululizo kwa Mtibwa kupoteza huku ukiwa mchezo wa tatu kwa ujumla ambao wanafungwa tangu kuanza kwa Ligi ya msimu huu na mchezo huu pia unakuwa mchezo pekee ambao umeshuhudia idadi kubwa ya mabao ambapo jumla ya mabao saba yalitinga wavuni mpaka kukamilika kwa dakika 90 za mechi.
Huu ni mchezo wa mwisho kwa Azam kabla hawajaingia uwanjani kucheza na timu ya El Mereikh ya nchini Sudan katika mzunguko wa kwanza wa michuano ya klabu bingwa barani Afrika utakaopigwa jumapili ya wiki hii.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook