Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amefanya ziara katika maeneo mbalimbali Jijini Dar es salaam kwa lengo la kujionea matokeo ya jitihada zilizofanywa na DAWASA katika kukabiliana na changamoto ya maji iliyokuwa ikiwakabili Wananchi wa Dar es salaam ambao sasa wameanza kupata huduma, ametembelea Sinza A, Manzese, Mabibo na maeneo mengine na kuahidi huduma kuimarika zaidi.
Mapema leo Waziri Aweso amefungua mtambo wa tenki la Chuo Kikuu kuruhusu maji kwenda maeneo ya Survey, Masaki, Mikocheni, Kawe, Tageta, Mbweni, Makumbusho, Kijitonyama, Mwananyamala na Mjini Kati,
Jana usiku kulifanyika pia zoezi la ufunguaji wa maji katika Bomba Kuu la usambazaji linaloelekea ukanda wa Magomeni baada ya kufungulia maji kutoka kwenye tenki ambapo huduma ya maji ilifika katika maeneo husika kwa muda wa saa 8 kuanzia saa 3 usiku ambayo ni Shekilango, Urafiki, Mabibo, Manzese, Sinza na Magomeni.
Baada ya zoezi hili Aweso ameingia mtaani kuhakikisha iwapo maeneo haya yamefikiwa na maji na kukutana na Wananchi waliothibitisha kuwa maji yapo tayari kwenye maeneo yao baada ya kukosekana kwa muda mrefu kutokana na kina cha maji kwenye chanzo cha maji kupungua kiasi cha kushindwa kusukuma maji kufika maeneo hayo.