Mgombea Urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt. John Pombe Magufuli, amesema kuwa jana alipita Jimbo la Kaliua wananchi wakamlilia kuhusu suala la ujenzi wa barabara ya lami ambapo aliwaambia sababu kubwa ni kuwa walikosea katika kuchagua wawakilishi wao.
Magufuli ametoa kauli hiyo leo Septemba 21, 2020, wakati akiomba kura kwa wakazi wa jimbo la Urambo mkoani Tabora, na kuongeza kuwa mradi wa maji ya kutoka Ziwa Victoria ukikamilika wilayani Urambo, atauhamishia Kaliua kwa kuwa anaamini mwaka huu hawatakosea.
“Uongozi haujaribiwi Kaliua walijaribu waliyaona katika miaka mitano iliyopita, nilifika pale jana wakaanza kuniambia barabara ya lami, barabara ya lami, kwani hamkuwaona hao mliokuwa mnawachagua, hayo ndiyo makosa makubwa yanayoweza kufanywa na wapiga kura” Magufuli
“Nataka wananchi wa Tabora waanze kuoga maji ya ziwani, nikasema kwamba mradi ukimalizika Urambo tutaupeleka Kaliua kwa sababu nina matumaini mwaka huu Kaliua hawatafanya makosa ambayo wameyafanya kwa miaka mitano iliyopita na wakifanya makosa muwaambie shauri yao” Magufuli