Upande wa Utetezi umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili vigogo wa Kampuni ya Mawasiliano ya Six Telecoms Limited, akiwemo Wakili maarufu Dk. Ringo Tenga, kuzungumza na wateja wao kuhusu kesi hiyo.
Hatua hiyo imekuja baada ya Upande wa Mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Constantine Kakula kudai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa shauri hilo limekuja kwa ajili ya kutajwa.
Kakula amedai Upande wa Utetezi wana jambo ambalo wanataka kuiambia mahakama hiyo.
Baada ya kueleza hayo, Wakili wa utetezi, Alex Mgongolwa aliiomba mahakama kuitisha shauri hilo Septemba 27 (Ijumaa hii) kwa sababu ya mazingira ya kesi yenyewe wanaomba wazungumze na wateja wao.
Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 27, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na washitakiwa wote wamerudishwa rumande kwa sababu mashitaka yanayowakabili hayana dhamana.
Julai 26, mwaka huu upande wa Utetezi uliowakilishwa na Wakili Bryson Shayo uliomba mahakama kuipangia kesi hiyo wiki mbili ili apate muda wa kushauriana na wateja wao.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Hafidhi Shamte au Rashidi Shamte ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa kampuni wa hiyo, Mfanyabiashara na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Peter Noni, Mkuu wa fedha wa kampuni hiyo Noel Chacha na Kampuni ya Six Telecoms.
Dk Tenga na wenzake wanadai kuwa, kati ya Januari 1, 2014 na Januari 14,2016 Dar es Salaam, walitoza maalipo ya mawasiliano ya simu za kimataifa chini ya kiwango cha Dola za Marekani 0.25 kwa dakika kwa lengo la kujipatia faida.
Pia katika kipindi hicho, wanadaiwa kuhujumu miundombinu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kutoza gharama chini ya kiwango na kushindwa kulipa kiasi cha Dola za Marekani 3,282,741.12 kwa TCRA, kama malipo ya mapato.
Vile vile ,washitakiwa hao wanadaiwa kuwa waliisababishia TCRA hasara ya Dola za Marekani 3,748,751.22 (sawa na Sh bilioni nane ).
RC TANGA AZUNGUMZIA WAKUU WA WILAYA KUTOELEWANA NA WAKURUGENZI