Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu aliyekuwa Rais wa TFF Jamali Malinzi na Katibu wake, Selestine Mwesigwa kulipa faini ya Shilingi Laki Tano ama kwenda jela miaka miwili.
Pia mahakama hiyo imemuachia huru Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga na Karani wa TFF, Flora Rauya kutokana na upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yao.
Hukumu ya Malinzi na wenzake ambao wamesota korokoroni kwa miaka 2 na Nusu imechukua takribani saa 5 ambapo ilianza kusomwa saa 8:30 mchana hadi saa 12 jioni.
Awali mahakama hiyo ilikwama kusoma hukumu hiyo kwa mara tatu mfululizo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo Hakimu aliyetakiwa kusoma hukumu hiyo kutokuwepo.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi, Maira Kasonde amesema amepitia ushahidi wa pande zote mbili baina ya utetezi na mashitaka ambapo amewatia hatiani washitakiwa katika makosa mawili kati ya 20.
“Kwa maana hiyo Mahakama inaona mshitakiwa wa kwanza na wa pili wana hatia kwa shitaka la tatu na mshitakiwa wa pili ana hatia katika shitaka la nne,”amesema.
Akitoa adhabu Hakimu Kasonde amesema;
“Shitaka la 3 ambalo ni kughushi nyaraka kila mshitakiwa anatakiwa kulipa faini ya laki 5 ama kifungo cha miaka miwili jela na kwa mshitakiwa wa pili katika kosa la nne la kuwasilisha nyaraka za uongo Benki anatakiwa kulipa faini ya Shilingi Laki Tano ama Jela miaka 2,” amesema.
Pia Hakimu Kasonde amesema mahakama hiyo imewakuta washitakiwa hao hawana hatia katika mashitaka 18 ikiwemo la utakatishaji fedha.
Awali kabla ya hukumu hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon aliiomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine.
Naye Wakili wa utetezi, Nehemia Nkoko amedai kuwa washitakiwa hao ni makosa yao ya kwanza kutenda na hawajawahi kushitakiwa.
“Pia mshitakiwa Malinzi anawatoto na amekamatwa akiwa na miaka 58 na sasa ana miaka 60, pia ana matatizo ya Kiafya,”
Kuhusu mshitakiwa wa pili, Wakili Nkoko amedai kuwa ana Mama wa miaka 89 anaumwa, pia ana mtoto wa miaka 4 na wakati anakamatwa alikuwa na miaka 47 hivyo na yeye anaelekea kwenye uzee.
“Tunaomba iwapatie unafuu wa adhabu,”amesema.
Awali kesi hiyo ilikuwa na mashtaka 30 lakini ilipofikia katika uamuzi wa kama washtakiwa wana kesi ya kujibu ama la walipunguziwa mashtaka 10 na kubakiwa na mashitaka 20.
Upande wa Jamhuri katika kesi hiyo ulikuwa na mashahidi 15 na vielelezo tisa.
Katika hatua hiyo mshtakiwa watano Miriam Zayumba aliachiwa huru kwa sababu alionekana hana kesi ya kujibu kwa mashtaka yote yaliyokuwa yakimkabili.
Kwa pamoja walikuwa wanakabiliwa na mashtaka 20 katika kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017.
Miongoni mwa mashitaka yao ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa Dola za Marekani 173,335.
Hata hivyo Malinzi na Mwesigwa wamerudishwa korokoroni kwa sababu ya kushindwa kulipa faini hiyo kwa siku ya leo, ambapo kesho Desemba 12, 2019 wanatarajia kulipa faini hiyo ili waachiwe huru.
PART 2: “Nimeachwa na Wanaume wawili Christmas, mmoja ameoa” (+video)