Shirikisho la Ngumi za kulipwa la Afrika (IBF Africa) kwa kushirikiana na Taasisi ya Miss Tanzania 2012, Brigitte Alfred Foundation (BAF) wameandaa mapambano ya ngumi ya kimataifa kwa kushirikisha mabondia nyota duniani.
Mapambano hayo yamepangwa kufanyika Novemba 28 kwenye ukumbi wa Mlimani City na lengo lake kubwa ni kutafuta fedha za kusaidia watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).
Akiongea na millardayo.com Miss Tanzania 2012 Brigitte alisema….“Tumeandaa mbio za Marathon mkoani Kilimanjaro wiki moja baada ya ngumi, mbio hizo, pia kutakuwa na zoezi la kupanda mlima Kilimanjaro, lengo ni kutafuta fedha za kuwasaidia albino na vile vile kutangaza utalii wetu, naomba makampuni yajitokeze,” -Brigitte.
Rais wa IBF Africa, Onesmo Ngowi alisema kuwa siku hiyo imepewa jina la “knock out albinos killers” (piga wanaua albino) ambapo bondia kutoka Denmark, Lolenga Mock atapigana na bondia nyota wa Zambia, Chioctha Chimwemwe katika pambano la uzito wa super middle la IBF continental Africa super.
Pambano hilo limepangwa kuwa la raundi 12 na litafuatiwa na pambano lingine la kulipiza kisasi kati ya bondia kutoka Afrika Kusini, Phillip Ndou atakayepambana na Mtanzania, Ramadhan Shauri kuwania ubingwa wa IBF-Continental Africa welterweight ambalo pia litakuwa la raundi 12.
Bondia nyota wa Tanzania, Cosmas Cheka naye atapanda ulingoni kupambana na Gottlieb Ndokosho wa Namibia kuwania ubingwa wa IBF continental Africa super-feather.
Waandaji wa tamasha hilo wameamua kushirikiana na Brigitte kutokana na kutambua juhudi zake za kutetea albino baada ya kuwajengea bweni eneo la Buhangija, Shinyanga na taasisi yake kwa kushirikiana na Junior Achievements (JA) wanatoa elimu ya ujasiriamali kwa jamii hiyo.
“Brigitte akiwa mwenye mashindano ya urembo ya dunia, 2012, aliweka rekodi ya kushika nafasi ya tatu katika mashindano ya ‘urembo wenye malengo maalum” au Beauty with purpose”, alipeleka kazi yake ya ujenzi wa bweni la albino mkoani shinyanga, imetupa faraja sana na kuamua kumuunga mkono katika vita hiyo,”- Onesmo Ngowi
PAPO KWA PAPO zipate habari zote zinazonifikia za siasa muziki, michezo, maisha, Breaking news na nyingine kwa kujiunga hapa na mimi >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos