Leo Mei 15, 2019 Mkurugenzi wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (UDART) Robert Kisena (46) na mkewe Frolencia Membe wamefutiwa mashitaka yao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kisha kukamatwa na kuunganishwa katika kesi moja yenye mashitaka 19 ikiwemo kusababisha hasara kwa UDART ya Bil.2.41.
Wawili hao pamoja na wenzao wengine watatu walikuwa wakikabiliwa na mashtaka tofauti ambapo walifutiwa mbele ya Mahakimu Thomas Simba na Augustine Rwizire.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Kulwa Kisena(33), Charles Newe(47) na raia wa China, Cheni Shi (32).
Kwa pamoja wamesomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizire na Wakili wa Serikali, Grory Mwenda ambapo amedai wanakabiliwa na mashitaka 19.
Katika mashitaka hayo yapo ya Kuongoza genge la uhalifu, kujenga kituo cha mafuta bila kibali, kuuza mafuta sehemu zisizoruhusiwa, Wizi wa mafuta na utakatishaji fedha wa Bil.1.2, kughushi na kusababisha hasara ya Bil.1.4.