Halmashauri ya mji wa Geita imeiomba Jumuiya ya Serikali za Mitaa nchini (ALAT) kupeleka kilio chao kwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI ili warudishiwe gari lao la kifahari lililochukuliwa na Serikali kwa madai ya kununuliwa kwa bei kubwa.
Gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser V8, lilichukuliwa na Tamisemi mwishoni mwa mwaka 2020 kufuatia malalamiko ya Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma kuwa gari hilo lilinunuliwa kwa bei ya Sh400 milion bila ridhaa ya madiwani, wakati kukiwa na na upungufu wa vyumba vya madarasa na vituo vya afya.
Hata hivyo, akizungumza leo Machi Mosi katika ziara ya viongozi wa ALAT taifa waliotembelea halmashauri hiyo, Mwenyekiti wa halmashauri ya mji, Constantine Morandi amesema wameandika barua kadhaa kudai gari hilo, lakini badala yake wamepatiwa gari jingine ambalo halilingani na thamani ya fedha ya awali.
“Badala ya kurudisha gari letu walitupa gari jingine ambalo sio jipya na limetembea kilometa 100,000 na hata bei yake sio ile. Basi waturejeshee fedha zetu au warejeshe gari lilelile,” amesisitiza Morandi.