Serikali ya Ghana imethibitisha uwepo wa kirusi Marburg nchini humo baada ya Wagonjwa wawili kugundulika kuwa walipatwa na virusi hivyo kabla ya kufariki siku chache zilizopita.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema vipimo vya awali vilibaini ugonjwa huo tarehe 10 July 2022 lakini vilipelekwa kuchunguzwa tena katika maabara nchini Senegal ambako pia majibu yalionesha matokeo hayohayo.
Idara ya Afya ya Ghana imesema inafanya juhudi kuhakikisha kuwa maradhi hayo hayasambai zaidi ikiwa ni pamoja na kuwatenga Watu wote waliosogeleana na Wagonjwa japokuwa hakuna yeyote miongoni mwao anayeonyesha dalili za maambukizi ya Marburg.
Hii ni mara ya pili kwa virusi hivyo kugunduliwa Afrika magharibi mara ya kwanza vilipatikana nchini Guinea mwaka jana lakini havikusambaa ambapo Wataalamu wanasema virusi vyake hupitishwa kwa Watu kutoka kwa popo wanaokula matunda huku dalili zake zikiwa ni maumivu ya kichwa, homa, maumivu ya misuli, kutapika damu na kutokwa damu na hadi sasa bado tiba yake haijapatikana.