Mahakama ya kimataifa inayoshughulikia kesi za makosa ya uhalifu wa kivita, ICC, imetangaza kuanzisha uchunguzi wa vitendo vya uhalifu wa kivita vilivyotekelezwa kwenye jimbo la Darfur nchini Sudan.
Katika tarifa yake, mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo, Karim Khan, amesema ofisi yake inaguswa na hali ya kuzorota kwa hali ya usalama kwenye êneo hilo pamoja na maeneo mengine ya nchi.
Tangazo lake limekuja miezi mitatu kupita tangu kuzuka kwa vita kwenye taifa hilo, Khan akiziambia nchi wanachama za baraza la usalama kuwa, ICC imekuwa ikichunguza uhalifu kwenye jimbo hilo tangu mwaka 2005, ambapo tayari imemshtaki rais wa zamani Omar Bashir kwa makosa ya mauaji ya halaiki.
Tuhuma za kutekelezwa vitendo vya ukatili kwenye êneo hilo, zimeripotiwa kwa uwingi baada ya kuzuka kwa vita, umoja wa Mataifa ukizituhumu pande zinazohasimiana kwa kuhusika na vitendo vya dhulma dhidi ya binadamu.
Hadi kufikia sasa watu zaidi ya elfu 3 wameripotiwa kuuawa huku wengine milioni 3 wakikimbia mapigano kati ya jeshi la Serikali na wapiganaji wa RSF.
ICC inasema miongoni mwa makosa yaliyoripotiwa kutekelezwa ni pamoja na mauaji ya kikabila, mateso, ubakaji na ukatili wa kijinsia.