Msanii wa vichekesho Idris Sultan amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi na wenzake wawili wakikabiliwa na kosa la moja la kichapisha maudhui mtandaoni bila kibali.
Washitakiwa wengine ni Daktari Ulimwengu na Isihaka Mwinyimvua.
Washtakiwa hao wamesomewa makosa yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi na Wakili wa Serikali, Batlida Mushi.
Katika kesi hiyo namba 60 ya mwaka 2020, Wakili Mushi amedai kuwa Idris na wenzake wametendeka kosa kati ya Machi 8, 2016 na Machi 12, 2020 katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam.
Inadaiwa katika maeneo hayo walirusha maudhui kupitia chaneli ya YouTube huku wakiwa hawana kibali cha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo, washitakiwa wote wamekana ambapo wakaachiwa kwa masharti ya dhamana ya kuwa na mdhamini mmoja kwa kila mshitakiwa ambao wamesaini bondi ya Sh.Mil 8 kila mmoja.
Kesi imeahirishwa hadi Aprili 21,2020 ambapo itarudi kwa ajili ya kusikilizwa.