Utawala wa kijeshi wa Myanmar umelitangaza kundi pinzani la Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuwa kundi la kigaidi na kulishutumu kuhusika na mashambulizi ya mabomu, uchomaji moto na mauaji. Kumekuwa na ripoti za mashambulizi ya kila siku ya mabomu huku makundi ya wanamgambo yakiundwa kukabiliana na jeshi.
Waandanamaji wanaopinga utawala wa kijeshi wameendelea na maandamano kote nchini humo na migomo ya kupinga mapinduzi imedhoofisha uchumi wa nchi.
Hapo jana Jumamosi maandamano yaliendelea katika maeneo kadhaa kupinga utawala wa kijeshi. Watu wapatao 774 wameuwawa na vikosi vya usalama na 3,778 wanashikiliwa kizuizini. Serikali ya Umoja wa kitaifa ambayo inaundwa na wabunge waliondolewa madarakani ilitangaza wiki hii kuanzisha jeshi la ulinzi wa wananchi.
Jeshi la Myanmar limekuwa likijaribu kurejesha utulivu tangu lipindue serikali ya kiraia mnamo Februari mosi na kumshikilia kiongozi wake Aung San Suu Kyi.