AyoTV

KESI YA BIL.1 :Maimu wa NIDA na wenzake waachiwa huru,wakamatwa tena(+video)

on

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachia huru Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA), Dickson Maimu na wenzake 6 kwa sababu Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hana nia ya kuendeleza mashtaka dhidi yao.

Washtakiwa hao wameachiwa chini ya kifungu cha 91(1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Mara baada ya kuachiwa vigogo hao waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na kusababisha hasara ya Sh.Bilioni 1.16 wamekamatwa tena.

Maombi ya DPP kuwaondolea mashtaka vigogo hao yamewasilishwa na Wakili wa Serikali, Wankyo Simon mbele ya Hakimu Mkazi Janeth Mtega.

Wakili Wankyo amedai kuwa DPP hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya washtakiwa hao, hivyo anawaondolea chini ya kifungu hicho.

Baada ya kuwaondolea mashtaka, Hakimu Mtega alikubali ombi hilo ambapo washtakiwa wakaachiwa lakini wakakamatwa tena na kupelekwa mahabusu.

Kesi hiyo ilifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani Agosti18, 2017 lakini hadi sasa upelelezi.

Washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo mbali na Maimu ni Meneja Biashara wa (NIDA), Avelin Momburi na Mkurugenzi wa TEHEMA, Joseph Makani.

Kwa pamoja washtakiwa walikuwa nane, lakini walibaki saba kwa sababu mmoja ambaye alikuwa Kaimu Mhasibu Mkuu wa NIDA, Benjamin Mwakatumbula alifariki dunia.

Wengine ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers, Astery Ndege, Ofisa Usafirishaji, George Ntalima, Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo.

Katika kesi hiyo, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ya kutumia madaraka vibaya, kula njama, kutumia nyaraka za uongo kumdanganya mwajiri na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh 1,169,352,931.

Inadaiwa kwenye shtaka la kwanza Maimu na Mwakatumbula kati ya Januari 15 hadi 19, mwaka 2010 katika makao makuu ya NIDA wilayani Kinondoni Mkoa wa Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma kwa nafasi walizokuwa nazo walitumia madaraka vibaya.

Wanadaiwa kuwa waliidhinisha malipo kwa Gotham International Limited (GIL) ya Dola za Marekani 2,700,00 bila ya kutumia viwango vya kubadilisha fedha za kigeni vilivyowekwa na Benki Kuu ya Tanzania, kinyume na kifungu 19.3 cha mkataba kati ya NIDA na GIL, hivyo kuifanya GIL kupata faida ya Sh 3,969,000.

ILIVYOKUWA KESI YA WATOROSHA DHAHABU NA ASKARI WALIOTAKA RUSHWA BILIONI 1

Soma na hizi

Tupia Comments