Baada ya wiki kadhaa zilizopita kupata mtikisiko wa migomo ya wafanyakazi wake, Shirika la ndege la Kenya limetangaza hasara ya shilingi bilioni 4.7 katika kipindi cha miezi sita kilichomalizika Septemba 30 mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa na shirika hilo la Serikali imesema pamoja na hasara hiyo bado kuna unafuu ikilinganishwa na ile ya shilingi bilioni 11.9 ambayo shirika hilo ilipata katika kipindi sawa na hicho mwaka 2016. Matokeo hayo yanaonyesha kuwa kampuni hiyo imepunguza pengo la hasara kwa asilimia 60.
Kupungua kwa hasara hiyo kumechangiwa na ongezeko la abiria waliotumia ndege za shirika hilo hadi kufikia abiria milioni 2.2 ikiwa ni ongezeko la asilimia 4 ambapo ni sawa na abiria elfu 89 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.
Taarifa hii imekuja wakati ambapo shirika hilo limekuwa likijaribu kila njia katika kukabiliana na changamoto mbali mbali ili kuboresha mapato yake.
Katika kipindi cha miezi sita iliyopita, shirika hilo lilipata mkopo wa shilingi bilioni 9.8 kutoka kwa serikali ya Kenya ili kufanikisha juhudi za kulikwamua kutoka kwa matatizo inayokabiliwa nayo.
ULIPITWA NA TAARIFA YA BENKI KUU KUHUSU KUICHUKUA BENKI YA TWIGA BANCORP? TAYARI IPO HAPA