Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Nchini (CGF) John William Masunga amewatunuku Maafisa na Askari wa Jeshi hilo Nishani 142 kutoka Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro pamoja na Tanga kwa Niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Chuo cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kilichopo Chogo, Wilayani Handeni Mkoani Tanga.
Akizungumza mara baada ya Kuwatunuku Nishani hizo Kamishna Jenerali Masunga amesema lengo la Nishani hizo ni katika Kutambua Utendaji kazi wa Maafisa na Askari wa Jeshi hilo pamoja na kuongeza Chachu ya Utendaji kazi katika kuongea ari na kujituma kwa Bidii zaidi.
Amesema Jukumu la Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ni kuokoa mali na Maisha ya Wananchi ambapo kumekuwa na Changamoto kadhaa ya Wananchi kulalamikia Jeshi kushindwa kufika kwenye matukio mbalimbali ambapo amesema sababu kubwa inayochangia ni Utoaji wa Taarifa kwa wakati.
Amesema majanga ya Moto yanapotokea kumekuwa na Tabia ya Wananchi kuanza kuzima moto wenyewe, na akiona Moto umezidi ndipo anaanza kupiga Simu kwenye kituo cha Zimamoto hali inayopeleka Moto kusambaa eneo kubwa hali ambayo imekuwa ni Changamoto
Kamishna Jenerali Masunga amesema Wajibu wa Mwananchi anapohitaji huduma za Uokoaji ni kutoa Taarifa mapema kwa Kupiga Namba 114 ambayo inapatikana Muda wote huku wakiwa wanaendelea na Juhudi za Kudhibiti moto huo