Ukiwa umepita mwaka mmoja tangu Manchester United ilipoanza kuwa chini ya kocha Mdachi Louis Van Gaal dalili za kocha huyo kuanza kuielekea njia ya mafanikio zimeanza kuonekana baada ya timu yake kuanza kufanya vizuri .
Hivi karibuni United imejikuta ikishika nafasi ya tatu kwenye ligi kuu ya England baada ya michezo miwili ikiwa imeshinda michezo dhidi ya Tottenham na Aston Villa na kujikusanyia pointi sita huku ikiwa haijaruhusu bao hata moja.
Moja ya mambo ambayo yamezungumzwa sana kwenye vyombo vya habari ni jinsi ambavyo United wanahitaji kuongeza nguvu kwenye eneo ya ulinzi ambapo wamekuwa sokoni wakiwasaka mabeki bora kama Sergio Ramos na Nicolas Otamendi .
Kauli ya United kuhitaji kuboresha idara ya ulinzi imepata nguvu zaidi baada ya kocha Louis Van Gaal kumchezesha kiungo wa kati Daley Blind kwenye eneo la ulinzi hali ambayo imewafanya wengi waamini kuwa anahitaji mtu kwenye nafasi hiyo.
Hata hivyo takwimu zinaongea kinyume na yale yanayozungumzwa na wachambuzi ambapo United inaonekana kuwa timu yenye safu borra ya ulinzi katika michezo iliyochezwa tangu mwezi Novemba .
United imeongoza kwa kufungwa idadi ndogo ya mabao ambapo tangu mwaka jana imefungwa mabao 23 pekee ikiwa mbele ya Chelsea ambayo Imeruhusu mabao 27 , takwimu hizi zimeanzia kwenye michezo 12 ya mwisho ya msimu uliopita mpaka michezo mitatu ya msimu huu ambapo katika michezo ya msimu wa mwaka 2015/2016 bado United haijaruhusu wavu wake kuguswa.
Chelsea imejikuta ikianza Ligi vibaya baada ya kufungwa kwenye mchezo mmoja huku ikitoka sare kwenye mchezo mwingine na hii leo (jumapili) vijana hawa wa Mourinho wanaingia uwanjani kucheza na West Bromwich Albion katika mechi ambayo matokeo yoyote tofauti na ushindi kwa Chelsea yatakuwa mabaya.