Mshereheshaji mmoja ameshindwa kuendesha sherehe ya harusi baada ya kubaini kuwa anayeolewa ni mpenzi wake wa zamani aliyempenda kwa dhati.
Tukio hilo limetokea Mwatate, Taita Taveta, nchini Kenya ambapo Mshereheshaji alilazimika kuachana na sherehe hiyo kwa kuwaachia kipaza sauti chao.
Mshereheshaji ambaye pia ni Mwalimu wa Shule ya Msingi aliachwa bila ugomvi na mpenzi wake huyo ambaye alikwenda kuolewa na Rubani.
“Heri niolewe na rubani, Mwalimu kama wewe unayekisifia Kiswahili chako na sauti nzuri utanipa nini?” jamaa alikumbuka mrembo akimuuliza na hapo akaishiwa nguvu mwilini na kuangusha kipaza sauti.
Aliinama akakiokota lakini akaanza kukohoa, hata maji aliyoletewa hayakumsaidia.
Hatimaye lofa aliamua kukabidhi mic akiashiria kwamba hangeendelea na sherehe, huku kisura akionekana akimtazama na kutabasamu akifurahia mateso ya jamaa.
“Alinikataa aolewe na jamaa yule mwenye sura ya nyani! jamani! kumbe pesa ni sabuni ya roho!” jamaa alisikika akisema huku akisaidiwa kuondoka jukwaani kwani alikuwa ameisha nguvu kabisa.