Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Jerry Muro ametoa mwezi mmoja kwa wanaume waliotelekeza watoto wilayani humo kuhakikisha wanaanza kutafuta watoto wao na kuanza kuwahudumia .
Dc Muro amesema baada ya muda aliotoa kuisha ataanza kuwakaribisha Wanawake wote wanaoishi wilayani humo waliotelekezewa watoto kupeleka Malalamiko yao ofisini kwake.
Muro alitoa maagizo hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya hali ya utelekezji wa watoto wilayani humo, amesema lengo la zoezi hilo ni kupunguza idadi ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu, hatarishi na wanaojihusisha na uhalifu na wale wanaozurura na kuzagaa mitaani kwa kukosa malezi ya Wazazi wawili.
“Nichukue fursa hii kuwataarifu akina mama na akina dada waliozalishwa na kutelekezewa watoto na kuachwa wabebe mzigo wa kuwahudumia watoto wako, natoa mwezi mmoja kwa kila mwanaume anayejua huko Arumeru aanze kutafuta mtoto aliyemtelekeza” amesema Muro
” Nitoe rai tu najua wako watu watakaokaidi naomba wajifunze kupitia zoezi lililofanyika DSM likiongozwa na RC Paul Makonda zoezi la Arumeru nitakuwa mkali zaidi kuliko la Dar, wajue zoezi limeisha huko na limetua Arumeru.”