Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la mto Sibiti litakalounganisha Mikoa ya Singida na Simiyu pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa jumla ya kilometa 25.
Daraja hilo lenye urefu wa meta 82 linajengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 20.172 na ujenzi wake unahusisha ujenzi wa nguzo kubwa 3 zenye kimo cha meta 7 kila moja, na pia linajengwa tuta lenye kimo cha meta 11 na makalvati 66.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema ujenzi huo umefikia asilimia 80 na kwamba utakamilika ifikapo mwezi Machi, 2018.
Akizungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi Rais Magufuli ameelezea kutoridhishwa na kasi ndogo ya ujenzi wa daraja hilo na ameitaka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na TANROADS kumsimamia mkandarasi kwa ukaribu ili ujenzi ukamilike haraka.
“Haiwezekani ujenzi wa daraja hili uchukue miaka 6 wakati wananchi hapa wanapata shida hasa wakati wa mvua, mkandarasi amelipwa fedha zote anazostahili nataka afanye kazi usiku na mchana, nataka nikirudi hapa nipite juu ya daraja, kama mkandarasi hawezi kumaliza kazi haraka mfukuzeni” Rais Magufuli.