Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemtia hatiani aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) David Mataka na aliyekuwa Kaimu Ofisa Mkuu Kitengo cha Fedha ambaye ni Askofu wa Kanisa la Pentecoste Motomoto, Elisaph Mathew.
Wawili hao wamehukumiwa kifungo cha miaka 6 jela ama kulipa faini ya Sh.milioni 70 ambapo Hakimu Mkazi Mkuu Victoria Nongwa, pia ameamuru watu hao kulipa hasara waliyoisababishia ATCL katika ununuzi wa magari chakavu 26 ambayo gharama yake ni zaidi ya milioni 300 za Kitanzania ambapo mshtakiwa wa kwanza ameshingwa kulipa faini na kupelekwa Gereza la Ukonga wakati mwenzie akitimiza masharti.
Aidha, Mahakama hiyo imewataka kugawana hasara waliyoisababisha ambayo ni dola za Marekani 143,442.75 na kuilipa kwa kipindi cha mwezi mmoja, huku Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Ndani, William Haji ambaye alikuwa mshitakiwa wa tatu katika kesi hiyo, ameachiwa huru kwa sababu hakupatikana na hatia.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa amesema mahakama imezingatia kigezo cha washitakiwa kuwa wakosaji wa kwanza na kwamba taratibu za utoaji wa adhabu zimeelekezwa na Mahakama Kuu ya kulipa faini au kifungo.
Katika kesi hiyo ambayo mashahidi walikuwa 14, Hakimu alisema katika mashitaka ya kwanza washitakiwa watatakiwa kulipa kila mmoja faini ya Sh milioni 5 au kifungo cha miaka mitatu huku katika mashitaka ya kutumia madaraka vibaya, wametakiwa kulipa faini ya Sh milioni tano kila moja na kosa la sita la kutumia madaraka vibaya, walipe Sh milioni 10 au kifungo cha miaka sita.
Kabla ya kutolewa adhabu, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi aliomba mahakama itoe adhabu stahiki kwa makosa ya kusababisha hasara na kwamba hawana rekodi ya makosa ya nyuma ya washitakiwa hao.
Akijitetea, Mattaka alidai anaishukuru mahakama kwa kuona wema wao wa kuiokoa ATCL mpaka walipofikia na kwamba taarifa walizonazo magari waliyonunua ndio yanayotumika hadi sasa kwani hawajaingiza mengine.
Pia alidai alipewa kazi hiyo na bodi ili kunusuru shirika na kwamba anamiaka 66 na anasumbuliwa na shinikizo la damu, ana familia inayomtegemea.
Mshitakiwa wa pili, Mathew alidai kuwa yeye ni Askofu wa Kanisa la Pentekoste hivyo akifungwa hataweza kuhubiri Injili ya Yesu Kristo na kwamba a naomba msamaha kwani anafamilia inayomtegemea.
Wakili wa utetezi, Francis Mgale alidai ni mara ya kwanza kwa mshitakiwa Mathew kufanya kosa hivyo mahakama impunguzie adhabu na iangalie mazingira yaliyowakuta ATCL hadi kutiwa hatiani.
Mattaka na mwenzake walishitakiwa mahakamani hapo kwa kwa mashitaka sita ikiwemo ya kula njama, matumizi mabaya ya madaraka na kulisababishia shirika hilo hasara ya dola 143,442.75 za Marekani.
Washitakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Machi na Julai 2007, wakiwa watumishi wa umma, walikula njama ya kutenda na kutumia madaraka yao vibaya kwa kuidhinisha ununuzi wa magari yaliyotumika 26 kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma.
Pia inadaiwa kati ya Juni na Julai 2007 wakiwa maofisa wa ATCL katika kutekeleza majukumu yao walikaribisha zabuni ya ununuzi wa magari 26 bila kufuata taratibu.
VIDEO: Spika Ndugai amwambie Zitto “Utanifanya nini? ninaweza kukuzuia usiongee hadi mwisho wa Ubunge wako” FULL VIDEO HAPA CHINI
.
HUTAKI KUPITWA?!!!! Ungana na MILLARD AYO kwenye mitandao ya jamii ili uzipate zote BREAKING NEWS, HABARI ZA MASTAA, VIDEO na mengine kabla hazijafika kokote…. BONYEZA HAPA >>> Youtube Facebook APP YA MILLARDAYO