Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amekutana na kufanya mazungumzo na wawekezaji kutoka Misri ambao wamefika hapa nchini kwa nia ya kuwekeza katika sekta ya ngozi na kukubaliana na baadhi ya mikakati ili uwekezaji watakaoufanya nchini uwe na tija kwao na taifa.
Akizungumza Jijini Dodoma, Naibu Waziri Ulega amesema ujio wa wawekezaji hao wakubwa nchini Misri, ambao umeongozwa na mshauri wa Waziri wa Viwanda na Biashara nchini Misri Mhandisi Yasser El Maghraby, umeonesha utayari mkubwa wa kuwekeza hapa nchini katika sekta ya ngozi kutokana na uwepo wa ngozi nyingi na bora.
“Tumepata wageni ambao wamekuja kuona maendeleo ya sekta ya ngozi nchini wawekezaji hawa ni wakubwa katika biashara ya ngozi nchini Misri, sisi kama taifa bado hatujafaidika vya kutosha na zao la ngozi” Ulega
“Tumekuwa tukizalisha takriban vipande vya ngozi ya ng’ombe milioni nne na mbuzi milioni tano kwa mwaka, lakini kuvibadilisha kuviweka katika bidhaa mbalimbali kama vile viatu, mabegi na mikanda bado ni changamoto na ngozi nyingi bado inaharibika katika maeneo ya vijijini kwa hiyo wenzetu hawa wamekuja kutuunga mkono.” Ulega
Naibu Waziri Ulega amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa jitihada anazozifanya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda vinavyochakata mazao ya wakulima, wafugaji na wavuvi.