Mahakama Kuu imetupilia mbali maombi ya Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu ya kufungua shauri la kutengua uamuzi wa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai uliosababisha kukoma kwa Ubunge wake Singida Mashariki.
Imesema Mwanasheria Mkuu huyo wa CHADEMA hakupaswa kuwasilisha maombi ya kutaka utenguliwaji wa Ubunge bali alitakiwa kufungua kesi ya kupinga Uchaguzi wa Ubunge katika Jimbo hilo.
Uamuzi huo umetolewa na Jaji Sirillius Matupa ambapo amesema maombi ya Lissu hayatekelezeki kwa sababu mleta maombi alitakiwa kufungua kesi ya kupinga Uchaguzi Mahakamani badala yake wameleta maombi ya kutaka kupinga uamuzi wa Spika.
Jaji Matupa amesema kama maombi ya Lissu yakikubaliwa yatasababisha uvunjaji wa Katiba kwa kuwa italazimika kuwa na Wabunge wawili kwenye jimbo moja na kwamba pia maombi hayo yemechelewa kufikishwa Mahakamani.