Leo Julai 24, 2019 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu kifungo cha miaka miwili jela Mhandisi, Novat Kaberwa baada ya kukiri kosa la kumuua mke wake, Clara Munisi bila kukusudia.
Kaberwa anadaiwa kumpiga mke wake na kumsababishia umauti baada ya kurudi nyumbani saa 3 usiku na kukuta watoto wameshinda njaa na mama yao (marehemu) kutokujulikana alipokwenda, kisha baadaye akarudi nyumbani akiwa amelewa kwa kutumia hela ya matumizi aliyoachiwa.
Hukumu imetolewa na Msajili wa mahakama, Pamela Mazengo, baada ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali na Wakili wa Serikali, Justus Ndibalema na kukubali kuwa alimuua mke wake bila kukusudia.
Katika maelezo ya awali aliyosomewa anadaiwa mshitakiwa alikuwa anaishi na Mke wake Clara maeneo ya Keko mwanga wilayani Temeke jijini Dar es Salaam.
Inadaiwa Januari 13,2016 majira ya jioni Clara alitembelewa na dada yake Veronika Munishi nyumbani kwake .
Alidai, Clara alimfahamisha dada yake huyo kuwa mume wake Kabelwa kuwa majira ya mchana alimpiga wakati huo mshtakiwa hayupo hapo nyumbani.
Baada ya hapo Clara na Veronika walienda dukani kununua mafuta ya kupikia wakati wanarudi nyumbani walimkuta mshtakiwa amerudi nyumbani ndipo ugomvi ulianza baina yao.
Wakati ugomvi ukiendelea Veronika alifanikiwa kukimbia wakati mshtakiwa akiendelea kumpiga mdogo wake Clara huku akimburuza na kumtoa nje ya geti ndipo marehemu akapiga kelele na majirani wakaja.
Kabelwa alipowaona majirani hao alikimbia ambapo walimchukua Clara na kumpeleka kituo cha Polisi na baadaye walimkimbiza katika hospitali ya Rufaa ya Temeke.
Inaelezwa kuwa hali ya Clara iliendelea kuwa mbaya na ilipofika Januari 14,2016 alifariki na mwili wake ulipelekwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi.
Januari 18,2016 uchunguzi wa mwili wa marehemu ulifanyika na ripoti ilionyesha sababu ya kifo chake damu ilivia tumboni.
Ilidaiwa kuwa, Januari 15,2016 Kabelwa alikamatwa eneo la Kilosa mkoani Morogoro na kuletwa kituo cha Polisi Chang’ombe.