Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirisha kesi ya uchochezi inayomkabili Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu hadi Septemba 23, 2019 kwa yupo nje ya nchi kimatibabu.
Wakili wa Serikali, Sylivia Mitando amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa shauri hilo limeitishwa kwa ajili ya kusikilizwa lakini mshtakiwa yupo nje ya Nchi kwa ajili ya matibabu, hivyo anaomba ahirisho.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Simba ameahirisha hadi Septemba 23, 2019 kwa ajili ya kusikilizwa.
Mbali ya Lissu washtakiwa wengine watatu ni Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh.
Kesi hiyo ilishafika katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka, lakini imeshindwa kuendelea kutokana na mshtakiwa wa nne katika kesi hiyo, ( Lissu )kuwa nchini Ubeljiji kwa ajili ya matibabu.
Kwa pamoja washtakiwa hao, wanadaiwa kuwa Januari 12 hadi 14, 2016 jijini Dar es Salaam, washtakiwa Jabir, Mkina na Lissu, waliandika na kuchapisha taarifaza uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’