Leo December 28, 2018 Rais Magufuli ameagiza kurejeshwa kwa utaratibu wa ulipaji wa mafao ya wafanyakazi wanaostaafu uliokuwa ukitumika kabla ya kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii, na ametaka utaratibu huo utumike mpaka mwaka 2023 wakati wadau wakijadiliana juu ya kikokotoo kitakachotumika kulipa mafao hayo bila kuathiri mfuko na wastaafu kulipwa vizuri.
Rais Magufuli amesikiliza maoni ya viongozi hao kuhusiana na utekelezaji wa Sheria ya Mfuko ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma namba 2 ya mwaka 2018 na kanuni zake ambapo viongozi hao wameelezea changamoto zilizojitokeza kwa wastaafu kulipwa kiasi kidogo cha fedha za mafao ya mkupuo na taharuki iliyowakumba wafanyakazi ambao ni wastaafu wa baadaye.
“Serikali hii haipo hapa kukatisha tamaa wafanyakazi, wala haipo hapa kuwaumiza wastaafu, kustaafu sio dhambi na mtu anayestaafu anatakiwa kuheshimiwa kwa sababu katika utumishi wake amejitolea kulitumikia Taifa lake kwa moyo wake wote, ameingia kazini akiwa kijana anaondoka amezeeka” amesisitiza Rais Magufuli.