Mtoto wa miaka 15 aliyekuwa akifanya kazi za ndani amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha akikabiliwa na shtaka la mauaji ya mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.
Amefikishwa mahakamani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Salome Mshasha huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili, Blandina Msawa .
Mtoto huyo amesomewa shtaka moja la mauaji ya kukusudia kinyume na sheria katika shauri ambalo halikuwa la wazi kutokana na umri wa mtuhumiwa.
Msawa ameieleza mahakama kuwa Juni 19, 2021 eneo la Olkerian kata ya Olasiti kinyume na sheria alimuua mtoto wa bosi wake kwa kumnyonga shingo na hakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 19, 2021 itakapotajwa tena kutokana na upelelezi wake kutokukamilika huku mtoto huyo akipelekwa gerezani.